i UHAKIKI WA WAANDISHI WA JINSIA TOFAUTI WANAVYOANGAZIA UKANDAMIZAJI WA KIJAMII KATIKA RIWAYA ZA MAISHA KITENDAWILI (JOHN HABWE: 2007) NA CHOZI LA HERI (ASSUMPTA MATEI: 2017) NA Maingi Nkoroi Nancy Tasnifu hii imetolewa ili kutosheleza baadhi ya mahitaji ya shahada ya uzamili (MA) katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya Machi 2024 ii UNGAMO Tasnifu hii ni kazi yangu binafsi na haijatolewa kwa mahitaji ya shahada katika chuo kikuu kingine. ______M. N. N__________________ _____03 – 03 - 2024______________ SAHIHI TAREHE MAINGI NKOROI NANCY Tasnifu hii imetolewa kutahiniwa kwa idhini yangu kama msimamizi aliyeteuliwa na Chuo Kikuu cha Mount Kenya. ____________________________ ______05/03/2024_________ SAHIHI TAREHE DKT. JACKLINE N. MURIMI CHUO KIKUU CHA TOM MBOYA iii IKISIRI IKISIRI Katika utafiti huu tumehakiki jinsi waandishi wa kiume na kike wanavyoangazia ukandamizaji wa kijinsia katika jamii kwa kurejelea riwaya za Chozi la Heri (Assumpta K. Matei) na Maisha Kitendawili (John Habwe). Utafiti huu unachunguza na kuchanganua kwa misingi ya kijinsia jinsi wahusika mbalimbali wanavyotengwa na kukandamizwa na jamii. Aidha, utafiti umechanganua jinsi waliotengwa na kukandamizwa na jamii wanavyosawiriwa katika macho ya waandishi wa kiume na wa kike. Isitoshe mapendekezo ya utatuzi wa matatizo haya yamedokezwa kwa kurejelea waandishi John Habwe na Assumpta K. Matei. Imebainika kuwa John Habwe amesawiri jinsia ya kike kama jinsia inayokandamizwa zaidi mikononi mwa yule wa kiume tofauti na Assumpta Matei ambaye ameangazia jinsia ya kiume kama jinsia iliyo na matatizo mengi ikilinganishwa na ile ya kike. Utafiti huu, uliongozwa na nadharia ya Jinsia - Hakiki iliyoasisiwa na mfeministi Showalter Elaine katika mwaka wa 1840. Nadharia hii hutumiwa kuhakiki kazi za kifasihi zilizoandikwa na watunzi wa jinsia tofauti tofauti. Data ya utafiti huu ilikusanywa kwa kutumia mbinu tatu mathalan utafiti wa maktabani ambapo tulisoma vitabu, majarida, matini na magazeti mbalimbali ili kukusanya data yetu. Pia tumesoma maandishi mbalimbali yanayolenga mada yetu hasa yale yaliyoandikwa na jinsia ya kiume na kike kuhusu ukandamizaji. Zaidi ya hayo, tumesakura mtandao ili kuweza kuelewa zaidi kuhusu kipengele cha ukandamizaji katika jamii. Tumetumia uteuzi wa sampuli wa kiamksudi katika kuteua riwaya ya Maisha Kitendawili na Chozi la Heri. Riwaya hizi mbili zimeandikwa na watunzi mwanamume na mwanamke ambao ni watunzi wa kazi za Kiswahili nchini Kenya. Tulikusanya data yetu kutoka kwa riwaya ya Maisha Kitendawili na Chozi la Heri. Aidha, tulipata data yetu kutoka mtandaoni, vitabuni, makala, maktabani na kwenye tasnifu. Tuliichanganua data yetu kwa kutumia maelezo na tarakimu, maelezo na ufafanuzi kuwasilisha data. Data hii ilitusaidia kutathmini kama waandishi wa jinsia ya kiume na kike wanaangazia masuala ya ukandamizaji kwa njia sawa ama kwa njia tofauti. Utafiti huu unanuiwa kunamfaa mwanafasihi katika kupata maarifa na uzoefu wa uhakiki kuhusu mwanajamii aliyetengwa na kuelewa kwa undani kazi mbalimbali zinazoangazia utetezi wa jinsia mbalimbali zilizotengwa katika jamii. Kazi hii vilevile inatusaidia katika kuangazia na kuweka wazi namna ambavyo waandishi wa kike na wa kiume wanavyochangia katika kushughulikia masuala ya ukandamizaji wa jinsia mbalimbali na mambo yanayohusu jamii tunamoishi. Isitoshe, utafiti huu unachangia katika kutoa suluhu ya namna mbalimbali za kushughulikia suala la kukandamizwa kwa jinsia mbalimbali. iv ABSTRACT This research has analysed how male and female writers highilight social oppression as shown in Maisha Kitendawili (John Habwe) and Chozi la Heri (Assumpta K. Matei). Specifically, this study has examined how various characters are marginalized and oppressed by society. This research is based on gender analysis on how different genders are seggragated and oppressed on equal measure by the society. This research has been guided by the tenets of the Gender Critique Theory that was put forth by Showalter Elaine (1840). This research has utilized quantitative methods. The data was collected by way of intensive reading of books, journals, online, papers and unpublished thesis related to the topic of research. Purposive sampling has been employed in this study. The data collected has been categorized, analyzed and explained and illustrated statistically in relation to the tenets of the theories and the objectives of the study. After analyzing the data, the findings have been presented through explanations, descriptive statistics and a summary given thereafter. The research findings have been able to utilize assess to whether male and female writers cover issues of oppression in the same way or in different ways. The research has come into conclusion that male writer John Habwe has potrayed female characters as oppressed more by their male counterparts as compared to those in Assumpta Matei’s novel. The writer Assumpta Matei has potrayed male character as a character who is facing a lot of oppression in the society as compared to the female character. As mentioned above the male writer has shown in his writing that the felame characters are oppressed more by their male counterparts as compared to the female writer who has shown the male character as a character who is being oppressed more by the society. This research is intended to benefit literature scholars to gain knowledge and expertise in analyzing issues pertaining to societal oppression in different works. This work also helps us to get a clear view of how male and female writers address social oppression and different issues affecting their societies. This research has offered solution on how to deal with different oppression affecting both male and female characters in the society. v TABARUKU Tasnifu hii naitabarukia wazazi wangu Albano Maingi na Jacinta Maingi, mume wangu mpendwa Lawrence Kirimi pamoja na wanangu Wayne Karani na Ariana Kinya. vi SHUKRANI Kwanza ninatoa shukrani zangu za dhati kwa Maulana kwa kuniwezesha kukamilisha kazi hii. Vilevile shukrani zisizo na kifani ni kwake msimamizi wangu Dkt Jackline N. Murimi kwa mawaidha na ushauri wake wenye busara na mwongozo wake mwema nilioufuata katika bahari hii ya kiusomi. Nampa hongera kwa namna alivyopitia sura mbalimbali ya kazi yangu kwa umakinifu wa hali ya juu ili niweze kuwasilisha kazi aali. Aidha, nawashukuru wahadhiri mbalimbali katika Idara ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya kwa ushauri wao wa kitaaluma. Mwongozo mlionipa katika harakati zangu za kujipatia shahada ya uzamili hauwezi kumithilishwa na chochote. Miongoni mwao ni Dkt Alex Umbima na Dkt Stanley Adika. Ustadi wenu na weledi wenu ulinitia moyo kutaka kuendelea tena na tena. Kwa wenzangu tulioabiri safari hii ya kiusomi pamoja Faith Kathure na Judy Muli ninawapa shukrani sufufu kwa kuwa tuliweza kuhimizana na kutiana moyo wakati hali haikuwa hali. Namshukuru sana Aloo R. kwa kunishika mkono wakati nilionyesha dalili za unyonge. Kwa wote walionisaidia kwa njia moja au nyingine nakushukuru sana tena mbarikiwe. vii UFAFANUZI WA ISTILAHI MUHIMU KATIKA UTAFITI HUU Jinsia ya kike – Sifa inayozibainisha nomino katika hali ya kike. Jinsia ya kiume – Sifa inayozibainisha nomino katika hali ya kiume. Nadharia – Taratibu, kanuni na misingi ambayo imejengwa katika muundo wa kimawazo kwa madhumuni ya kutumiwa kama kielezi cha kuelezea jambo. Nadharia ya Jinsia – Hakiki – Taratibu, kanuni na misingi inayotumiwa katika kuhakiki historia ya kifasihi ya watunzi wa jinsia mbalimbali. Ufeministi – Dhana iliyo na msingi kutokana na misukumo mikubwa pamoja na nia ya kupigania ukombozi wa jinsia ya kike kutokana na pingu za kiutamaduni, kijamii, kidini, kiuchumi na kisiasa. viii VIFUPISHO NACOSTI - Tume ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Uvumbuzi. NACADA – The National Authority for the Campaign Against Alcohol and Drug Abuse. TUKI – Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili. ix YALIYOMO UNGAMO ...................................................................................................................................... ii IKISIRI ......................................................................................................................................... iii IKISIRI ......................................................................................................................................... iii ABSTRACT .................................................................................................................................. iv TABARUKU .................................................................................................................................. v SHUKRANI .................................................................................................................................. vi UFAFANUZI WA ISTILAHI MUHIMU KATIKA UTAFITI HUU .................................... vii VIFUPISHO ............................................................................................................................... viii SURA YA KWANZA ................................................................................................................... 1 1.0 Utangulizi ........................................................................................................................ 1 1.1 Usuli wa Mada ..................................................................................................................... 1 1.2 Suala la Utafiti ..................................................................................................................... 4 1.3 Malengo ya Utafiti ............................................................................................................... 4 1.4 Maswali ya Utafiti ............................................................................................................... 5 1.5 Sababu ya Kuchagua Mada Hii ......................................................................................... 5 1.6 Umuhimu wa Utafiti ........................................................................................................... 6 1.7 Upeo na Mipaka ya Utafiti ................................................................................................. 7 1.8 Msingi wa Kinadharia ........................................................................................................ 8 1.9 Hitimisho ............................................................................................................................ 10 SURA YA PILI ............................................................................................................................ 11 MAPITIO YA MAANDISHI ..................................................................................................... 11 2.1 Utangulizi ........................................................................................................................... 11 2.2 Yaliyoandikwa Kuhusu Mada ......................................................................................... 11 2.3 Hitimisho ............................................................................................................................ 20 SURA YA TATU ......................................................................................................................... 21 MBINU ZA UTAFITI................................................................................................................. 21 3.0 Utangulizi ........................................................................................................................... 21 3.1 Muundo wa Utafiti ............................................................................................................ 21 x 3.2 Wango la Utafiti ................................................................................................................ 21 3.3 Uteuzi wa Sampuli ......................................................................................................... 22 3.4 Eneo la Utafiti .................................................................................................................... 22 3.5 Ukusanyaji Data ............................................................................................................ 22 3.6 Uchungunuzi wa Data ................................................................................................... 23 3.7 Maadili ya Utafiti .............................................................................................................. 23 3.8 Hitimisho ............................................................................................................................ 24 SURA YA NNE ........................................................................................................................... 25 UCHANGANUZI WA DATA NA UFASIRI WA MATOKEO YA UTAFITI ..................... 25 4.0 HISTORIA YA JOHN HABWE, ASSUMPTA MATEI NA AINA MBALIMBALI ZA UKANDAMIZAJI KATIKA MAISHA KITENDAWILI NA CHOZI LA HERI ................... 25 4.1 Utangulizi ........................................................................................................................... 25 4.2 Waandishi Wanaume na Wanawake .............................................................................. 25 4.3 Historia ya John Habwe ................................................................................................... 26 4.4 Historia ya Assumpta Matei ............................................................................................. 29 4.5 Muhtasari wa Riwaya ya Chozi la Heri ........................................................................... 30 4.6 Muhtasari wa Riwaya ya Maisha Kitendawili ................................................................. 30 4.7 Aina Mbalimbali za Ukandamizaji wa Jinsia Tofauti Tofauti katika Riwaya ya Maisha Kitendawili na Chozi la Heri ...................................................................................... 31 4.7.1 Utangulizi .................................................................................................................... 31 4.7.2 Ukandamizaji wa Kijinsia katika Maisha Kitendawili ............................................ 44 4.8 Namna Waandishi wa Kiume na wa Kike Wanavyokabiliana na Ukandamizaji katika Jamii Katika Riwaya ya Chozi la Heri na Maisha Kitendawili ............................................ 59 4.8.1 Malezi ........................................................................................................................... 59 4.8.2 Elimu ............................................................................................................................ 61 4.8.3 Dini ............................................................................................................................... 62 4.9 Hitimisho ............................................................................................................................ 63 SURA YA TANO ........................................................................................................................ 65 MUHTASARI, HITIMISHO NA MAPENDEKEZO ............................................................. 65 5.0 Utangulizi ........................................................................................................................... 65 5.1 Muhtasari wa Utafiti ......................................................................................................... 66 5.2 Hitimisho ............................................................................................................................ 70 xi 5.3 Mapendekezo ya Utafiti Zaidi .......................................................................................... 70 Marejeleo ..................................................................................................................................... 70 KIAMBATISHO 1: BARUA YA NACOSTI ........................................................................... 74 KIAMBATISHO 2: BARUA YA UTANGULIZI .................................................................... 75 1 SURA YA KWANZA 1.0 Utangulizi Sura hii inatoa ufafanuzi wa kimsingi unaohusu usuli wa mada ya utafiti, tatizo la utafiti wetu, malengo ya utafiti huu, maswali yanayohusu utafiti huu, sababu ya kuchagua mada hii, umuhimu wa utafiti, upeo na mpaka wa utafiti huu, msingi wa kinadharia wa utafiti huu, yaliyoandikwa kuhusu mada ya utafiti huu, mbinu mbalimbali za utafiti na maadili ya utafiti. 1.1 Usuli wa Mada Waandishi wanaume na wa kike wamekuwa wakibuni kazi mbalimbali kwa kipindi kirefu. Aidha, watafiti wengi wamekuwa wakifanya utafiti kuhusu suala la jinsia na uandishi wao ili kubainisha iwapo uandishi wa mwanamume ni tofauti na ule wa mwanamke. Kwa mujibu wa Eagleton (1986), si lazima mwandishi wa jinsia ya kike akiandika kazi yoyote ya kifasihi iwe inaakisi hali zinazokumba jinsia ya kike. Isitoshe, mwandishi wa jinsia ya kike lazima ajitenge na hisia zake anapoandika kama njia ya kufanya kazi hiyo iwe yakinifu. Eagleton anasisitiza kuwa kupitia njia hii, huenda tofauti bayana ikadhihirika kati ya mwandishi wa jinsia ya kike na yule wa kiume. Waandishi wa jinsia ya kiume na wale wa kike huangazia masuala mbalimbali ambayo yanakumba jamii kwa njia maalum. Aidha, kwa njia hii, watunzi hawa huwajenga wanaodhulumiwa katika jamii na kuwakuza kwa namna inayoonyesha mguso kama njia ya kuwateka wasomaji. Wanaunda mazingira mapya katika fasihi ambazo wanaandika na hata kutumia mbinu zinazomteka msomaji. Baarret (1986) anaeleza kuwa kuna tofauti kubwa katika uandishi wa jinsia ya kike na ule wa kiume. Anaendeleza mjadala huu kwa kusisitiza kuwa uandishi wa jinsia ya kiume ni wa kawaida tofauti na uandishi wa jinsia ya kike. Kwa mfano, lugha inayotumiwa na jinsia ya kike imejaa hisia tele tofauti na lugha ya jinsia ya kiume ambayo ina uthabiti. Kwa ujumla waandishi wa jinsia 2 totafuti tofauti hutofautiana kiuandishi kwa vile wana hali tofauti, vilevile wanaishi katika utamaduni tofauti. Waandishi wa jinsia ya kike hujadili kwa upekee matatizo ambayo hukumba jamii ikilinganishwa na wale wa kiume. Hivyo basi watunzi hawa wawili husawiri wanaokandamizwa na jamii kwa njia tofauti huku wakiwakuza na wakiwavutia wasomaji wao kwa njia tofauti. Watunzi hawa huunda ulimwengu mpya na kuwateka wasomaji wao kwa kutumia mbinu tofauti tofauti. Kazi za Woolf (1929) na Wollstonecraft (1792) ni moja kati ya kazi za kwanza ambazo zilitoa michango mikubwa katika kuzindua harakati za ukombozi wa jinsia mbalimbali katika jamii. Kwa upande mwingine Simon de Beauvoir alipiga hatua zaidi katika kushughulikia ukandamizaji wa jinsia tofauti tofauti katika jamii katika kazi yake ambayo inaitwa The Second Sex (1949). Mtafiti huyu aliuchukua mtazamo wa kiharakati. Katika kazi yake ameshughulikia asasi mbalimbali za kijamii ambazo zinachangia udhalilishaji ama udunishaji wa jinsia mbalimbali katika jamii. Baadhi ya asasi alizozitaja ni pamoja na; dini, utamaduni na ndoa. Simone de Beauvoir (1949) alikashifu mtazamo wa kiutamaduni ambao uliangalia jinsia ya kike kama kiumbe duni na kumwona jinsia ya kiume kama kielelezo katika jamii. Anaeleza kuwa utamaduni ambao wanakulia jinsia mbalimbali huchangia katika kuwadunisha hadi katika hali ya unyonge. Kwake Simon de Beauvoir, utamaduni unaweza kumlazimisha jinsia fulani kukubali kuwa kiumbe duni. Hivyo kufanya jinsia hiyo kukubali kuwa anaishi kama chombo ambacho kinatumiwa kuendeleza mifumo hasi ya kijamii. Asasi ya pili aliyoshughulikia ni asasi ya ndoa. Simon de Beauvoir anasema kuwa asasi hii hutumiwa kuwakandamiza jinsia mbalimbali. Kwa mfano asasi hii inasisitiza uwezo mkubwa 3 iliyonayo jinsia ya kiume dhidi ya jinsia ya kike. Kwake, jinsia ya kike anaonekana kama chombo. Isitoshe, asasi hii pia inasisitizwa na matamko mbalimbali ya kidini ambayo humweka jinsia ya kike chini ya utawala wa jinsia ya kiume. Ellman (1970) katika kazi yake Thinking about Women alishughulikia namna ambavyo jinsia ya kike ameelezwa katika kazi ambazo zimeandikwa na jinsia ya kiume. Aidha, ameangazia namna baadhi ya waandishi wa kike wanavyoendelea kuwasawiri wanawake wenzao kwa njia hasi katika kazi wanazoandika. Millet (1970) katika kazi yake Sexual Politics anasema kuwa muundo wa jamii na asasi za kijamii hushirikiana katika kuwakandamiza jinsia mbalimbali. Millet anasema kuwa wivu wa jinsia ya kike husababishwa na uwezo mkubwa aliopewa jinsia ya kiume na jamii. Hata hivyo watafiti mbalimbali wanakubaliana kuhusu mambo mbalimbali yanayohusiana na ukandamizaji katika jamii. Wanasisitiza kuwa jinsia mbalimbali wanakandamizwa na hata kunyimwa haki zao na jamii iliyo na mifumo ambayo inadhibitiwa na jinsia tofauti tofauti. Wanaeleza kuwa kuna haja ya jinsia mbalimbali kuungana ili wapiganie uhuru wao. Steady (2004) anafikiria kuwa labda dhana ya usawa wa kijinsia haitoshi kuelezea hali ya jinsia mbalimbali kwa ukamilifu. Anarai kuwa iwapo kauli hii itakubalika, itabidi jinsia mbalimbali waungane ili usawa huo ufikiwe. Hata hivyo, anasisitiza kuwa suala hili ni nadra sana kutokea. Steady (2004) anakariri kuwa suala kama vile uana, utabaka na rangi ni misingi ya utofauti baina ya jinsia mbalimbali. Mnamo mwaka wa 1970, miungano ya kupigania haki za kijinsia kule Ulaya ilishindwa kukubaliana ikiwa ukosefu wa usawa baina ya jinsia unasababishwa jinsia au uana. Wataalamu 4 kama vile Anfred (2004) walishindwa kukubaliana iwapo mabadiliko ya kisheria au siasa ama mabadiliko ya kijamii ndiyo yataweza kutatua migogoro iliopo baina ya jinsia mbalimbali. Utafiti huu unahakiki suala la usawiri wa ukandamizwaji kupitia kwa kulinganisha riwaya mbili tofauti zilizoandikwa na mwandishi wa kiume na yule wa kike. Hivyo basi, ninatumia riwaya mbili za jinsia ya kiume na kike zilizotungwa katika karne ya ishirini na moja; Maisha Kitendawili (John Habwe: 2007) na Chozi la Heri (Assumpta Matei: 2017). 1.2 Suala la Utafiti Usawiri wa wahusika na matatizo katika jamii hushughulikiwa kwa njia tofauti na waandishi wanaume na wale wa kike. Inadaiwa kuwa waandishi wanawake hushughulikia kwa undani zaidi masuala ambayo ni nyeti na hata kuwasawiri wahusika wao kwa njia ambayo inateka hisia za wasomaji. Inaaminiwa kuwa watu ambao wanatengwa na kudhulumiwa na jamii zaidi ni wanawake. Hivyo basi, utafiti huu unachanganua jinsi wahusika mbalimbali waliotengwa na kukandamizwa na jamii wanavyosawiriwa katika macho ya waandishi wanaume na wanawake kwa kurejelea kazi za John Habwe na Assumpta K. Matei. 1.3 Malengo ya Utafiti Utafiti huu uliongozwa na malengo manne yafuatayo: i) Kubainisha aina mbalimbali za ukandamizaji zinazoendelezwa katika jamii katika riwaya ya Maisha Kitendawili na Chozi la Heri. ii) Kuchanganua wanaoendeleza aina mbalimbali za ukandamizaji katika riwaya ya Maisha Kitendawili na Chozi la Heri. 5 iii) Kutathmini jinsi mwandishi wa jinsia ya kiume na mwandishi wa jinsia ya kike wanavyolijadili na kusawiri wahusika waliokandamizwa na jamii katika riwaya ya Maisha Kitendawili na Chozi la Heri. iv) Kujadili namna ya kukabiliana na ukandamizaji katika jamii kwa mujibu wa riwaya ya Maisha Kitendawili na Chozi la Heri. 1.4 Maswali ya Utafiti Utafiti huu uliongozwa na maswali yafuatayo: i) Je, ni aina zipi za ukandamizaji zinazoendelezwa katika jamii katika riwaya ya Maisha Kitendawili na Chozi la Heri? ii) Je, aina mbalimbali za ukandamizaji zinaendelezwa na nani katika riwaya ya Maisha Kitendawili na Chozi la Heri. iii) Je, mwandishi wa jinsia ya kiume na mwandishi wa jinsia ya kike wanajadili na kusawiri vipi wahusika waliokandamizwa na jamii katika riwaya ya Maisha Kitendawili na Chozi la Heri? iv) Je, ukandamizaji wa aina mbalimbali unaweza kukabiliwa kivipi katika jamii kwa mujibu wa riwaya ya Maisha Kitendawili na Chozi la Heri. 1.5 Sababu ya Kuchagua Mada Hii Kazi mbalimbali katika utanzu wa fasihi huangazia masuala mbalimbali ambayo yanaathiri jamii kama vile ubabe wa kiume kwa mwanamke na dhuluma dhidi ya jinsia ya kike. Kazi mbalimbali zinazozungumzia masuala yanayoathiri jamii huegemea sana upande wa dhuluma dhidi ya jinsia ya kike. Kazi hizi hazijashughulikia namna jinsia ya waandishi wa kiume na wale wa kike 6 wanavyoangazia wanajamii mbalimbali wanaokandamizwa. Kwa vile kipengele cha jinsia ya kike kimeangaziwa sana katika uhakiki mbalimbali za kifasihi kuna haja ya kuangazia jinsi waandishi wa kiume na wale wa kike wanavyoshughulikia vipengele vingine ambavyo vinawaathiri wanajamii. Kwa kuwa tafiti nyingi zinaonyesha kuwa jinsia ya kike imekandamizwa zaidi na kupewa nafasi ya pili baada ya jinsia ya kiume, tutachunguza namna jinsia tofauti tofauti wanavyosawiriwa na waandishi wa jinsia ya kike na wale wa kiume kupitia kwa ukandamizaji wa aina mbalimbali za kijamii kwa kuwa uwanja huu umetafitiwa na wahakiki wachache sana kufikia sasa. Isitoshe, tumewachagua mwandishi mwanamke na mwanamume kwa ajili ya kuchunguza kama wameangazia ukandamizaji wa jinsia mbalimbali kwa ujumla. Utafiti huu ulinuia kujaza pengo kwa kuonyesha changamoto ambazo huwapata wanajamii na wanaosababisha ukandamizaji huo kwa kunaangazia namna tunavyoweza kupata suluhisho ili kutatua ukandamizaji huu. Zaidi ya hayo, utafiti huu tuliuchagua kwa sababu tafiti nyingi za hapo awali zimechunguza pakubwa masuala yanayohusu ukandamizaji wa jinsia ya kike na kwa uelewa wetu hadi sasa hatujapata tafiti zinazolinganisha namna jinsia ya kiume na kike wanavyolinganisha ukandamizaji wa kijamii. Mwisho, utafiti huu unapanua mitazamo ya kuchunguza wanajamii wanaokandamizwa kupitia kwa waandishi wa jinsia ya kike na wale wa kiume Kazi zilizoteuliwa ni za hizi majuzi na hivyo watunzi wake wanashughulikia masuala ambayo yanazikumba jamii za kisasa. 1.6 Umuhimu wa Utafiti Utafiti huu unamfaa mwanafasihi katika kupata maarifa kuhusu mwanajamii aliyetengwa na kuelewa kwa undani kazi mbalimbali zinazoangazia utetezi wa jinsia mbalimbali zilizotengwa 7 katika jamii. Kazi hii vilevile inatusaidia katika kuangazia na kuweka wazi namna ambavyo waandishi wa kike na wa kiume wanavyochangia katika kushughulikia masuala ya ukandamizaji wa jinsia mbalimbali na mambo yanayohusu jamii tunamoishi. Isitoshe, utafiti huu unachangia katika kutoa suluhu ya namna mbalimbali za kushughulikia suala la kukandamizwa kwa jinsia mbalimbali. Utafiti huu unachangia ufundishaji wa Kiswahili kwa kubainisha namna waandishi mbalimbali wanavyoangazia suala la ukandamizaji katika jamii, utatuzi wake na ujumbe unaopatikana kutokana na ukandamizaji wa kijamii. Kadhalika, utafiti huu unawaongezea wanafasihi uzoefu katika uhakiki wa kazi mbalimbali zinazoangazia ukandamizaji katika jamii. 1.7 Upeo na Mipaka ya Utafiti Kuna riwaya kadha wa kadha za Kiswahili zinazoangazia masuala ya ukandamizaji na kutengwa kwa jinsia mbalimbali katika jamii. Hata hivyo, tumeteua riwaya mbili tu ambazo ni Maisha Kitendawili na Chozi la Heri. Riwaya hizi zimeandikwa na jinsia ya kiume na kike ili kuhakiki namna watunzi hawa wa jinsia hizi tofauti wanavyoangazia suala la ukandamizaji katika jamii. ninashughulikia waliokandamizwa kielimu, kisosholojia, kisaikolojia, kiutamaduni, kiuchumi, kiuongozi na kijinsia. Utafiti unaangazia vipengele hivi kama njia ya kuonyesha namna taasisi mbalimbali za kijamii zinavyoendeleza unyanyapaa baina ya wanajamii. Ingawa kuna kazi nyingi katika lugha ya Kiswahili zinazoangazia suala la ukandamizaji katika jamii, katika utafiti wetu, riwaya ya Maisha Kitendawili ya John Habwe (2007) na Chozi la Heri ya Assumpta K. Matei (2017) zitafaa zaidi katika utafiti wetu, kwa sababu riwaya hizi zinanisaidia katika kuafikia malengo yetu ya utafiti. Aidha, kazi hizi ni za karibuni na zimeangazia masuala ya ukandamizaji kwa mapana. 8 1.8 Msingi wa Kinadharia Utafiti huu uliongozwa na Nadharia ya Jinsia - Hakiki ambayo iliasisiwa na mfeministi Showalter Elaine katika mwaka wa 1840. Nadharia hii hutumiwa kuhakiki kazi za kifasihi zilizoandikwa na watunzi wa jinsia tofauti tofauti. Kwa mujibu wa Showalter, nadharia hii hutumiwa katika kuhakiki historia ya kifasihi ya watunzi wa jinsia mbalimbali. Anasisitiza kuwa kuna tofauti kubwa kati ya uandishi wa jinsia ya kiume na jinsia ya kike kwa kuwa watunzi wa jinsia ya kike huwa wanashughulikia matatizo ambayo ni ya kimsingi na kuwa matatizo haya hupuuzwa na watunzi wa jinsia ya kiume. Bali na nadharia hii kushughulikia jinsia, nadharia hii vilevile huangazia mawazo ya kindani ya jinsia mbalimbali. Showalter anasisitiza kuwa hadi karne ya ishirini kumekuwepo na taasubi ya kiume iliyojaa miongoni mwa wanajamii hivyo basi taswira na maadili ya jinsia ya kike imejengeka kwa mitazamo ya kifeministi sawa na utamaduni wa fasihi ya jinsia ya kike. Vilevile nadharia hii ilichipuka kutokana udadisi-saiko wake Sigmund Freud. Nadharia ya Jinsia - Hakiki ilichipuka kutoka kwa nadharia ya Ufeministi. Maendeleo ya nadharia hii yametokea katika awamu tatu. Awamu ya kwanza ni ‘awamu ya kike’ ambayo ilianza kati ya mwaka wa 1840 hadi 1880. Awamu hii iliuhusishwa pakubwa na Gaskell Elizabeth na Eliot George. Kulingana na Showalter, wakati huu kulikuwa na watunzi wengi wanaume huku wale waandishi wa kike wakiwekwa pembeni. Aidha, walikuwa wamewekewa vikwazo kwa kuandika kazi za kifasihi zilizohusishwa na hali ya kijamii ambazo zinalingana na utamaduni wa jamii husika. Awamu ya pili ilikuwa na wahakiki kama vile Robins Elizabeth na Schreiner Olive. Awamu hii ilianzishwa kati ya mwaka 1880 hadi 1920 na ni hawamu iliyojulikana kama ‘awamu ya 9 ufeministi’. Wahakiki ambao wanahusishwa na awamu ya mwisho ni Mansfield Katherine na Rebecca West. Awamu hii ilirejelewa kama ‘awamu ya mwanamke’. Mhakiki Carol (1986) anaendeleza nadharia ya Jinsia Hakiki kwa kusema kuwa inainua jinsia ya kike na kumweka katika mizani sawa na jinsia ya kiume. Kwake, jinsia ya kike akibainishwa chini ya utambuaji wa mwandishi mwanamke ni sawa na kumdunisha kwa kuwa hakuna utambuzi wa mwandishi wa jinsia ya kiume. Kwa mujibu wa mhakiki huyu, uandishi wa kawaida ni wa jinsia ya kiume hata kama jinsia hii haijatambulishwa hivyo. Carol anasisitiza kuwa utambuzi wa aina hii haufai kutokea. Isitoshe, nadharia hii ya Jinsia – Hakiki itatusaidia katika kuleta usawa na nguvu sawa kati ya mwandishi wa jinsia ya kike na yule wa jinsia ya kiume. Jacobus (1986) katika kitabu chake The Difference of View: Women Writing and Writing about women anadai kuwa Nadharia ya Jinsia Hakiki huwasilisha uandishi wa kazi ya jinsia ya kike kama uandishi unaoendeleza furaha kuliko kutengwa kwa wale ambao wananyanyaswa na jamii. Mhakiki huyu anaendelea kwa kusema kuwa katika vipindi vya hivi karibuni ambapo jinsia ya kike amepata uhuru wa kujikomboa na kujieleza kutoka kwa pingu za jinsia ya kiume. Mtunzi wa jinsia ya kike anaweza kutumia uandishi wake ili kuonyesha ushindi wa watu waliotengwa hata kama wananyanyaswa. Showalter anaelezea kuwa uhakiki wa Jinsia – Hakiki unaendeleza kwa mapana uhakiki wa kazi zilizoandikwa na jinsia ya kiume na wale wa kike. Mhakiki huyu anathamini mwandishi wa kazi ya kifasihi kuliko kile ambacho mwandishi huyu amekiandika kwa sababu kwanza wanachunguza aliyetunga kazi inayohusika. Wanahakiki kazi kwa kutumia macho ya jinsia ya kike, vilevile wao huelewa kazi kupitia kwa jinsia ya mwandishi husika. Uafiti huu umetumia nadharia hii ili kuelewa namna watunzi hawa wa kike na wa kiume wanavyoandika na namna wanavyowasawiri wahusika tofauti tofauti hasa wale waliotengwa na 10 hata kukandamizwa. Nadharia hii ni muhimu katika kuonyesha upekee wa mwandishi wa jinsia ya kike na yule wa jinsia ya kiume anapojenga ulimwengu wa kifasihi katika kazi ambazo wanaziandika. Utafiti huu wa Jinsia Hakiki unaongozwa na mihimili hii: i. Historia ya fasihi ya mwandishi wa jinsia ya kiume na yule wa kike. ii. Kushughulikia matatizo ya kimsingi yanayowakumba mtunzi wa jinsia ya kiume na wa kike hayaepukiki. iii. Uendelezaji wa kufurahia zaidi ya utengano. iv. Kuonyesha ushindi kwa wale ambao wametengwa katika jamii hata ikiwa wanadhulumiwa. v. Kuonyesha jinsia mbalimbali ambao wametengwa. Mihimili hii inasaidia katika kuendeleza utafiti na hata kuhakiki data ya utafiti huu. Mihimili hii inasaidia katika kutambua matatizo yanayokumba jinsia mbalimbali. Utafiti huu umeweza kubainisha ukandamizaji wa aina mbalimbali unaotokea katika riwaya ya John Habwe na ya Assumpta Matei kupitia kwa mihimili hii. Vilevile tumeweza kutambua jinsi taasisi mbalimbali zinavyotatua ukandamizaji sawa na uliotokea katika riwaya hizi na hata kupendekeza mbinu za kimsingi zinavyoweza kutumiwa katika jamii ili kuzuia ukandamizaji katika jamii. 1.9 Hitimisho Sura hii imeangazia utangulizi mfupi kuhusu kazi yetu. Vilevile nimeshughulikia vipengele mbalimbali vya sura hii na namna vipengele hivyo vitakavyotuongoza katika utafiti wetu. Aidha, utafiti umeshughulikia umuhimu wa utafiti katika somo la Kiswahili. Zaidi ya hayo utafiti umezungumzia nadharia ya utafiti ambayo ni Jinsia- Hakiki na mihimili wa nadharia hii. 11 SURA YA PILI MAPITIO YA MAANDISHI 2.1 Utangulizi Sura hii imeangazia mambo mbalimbali yaliyoandikwa na wahakiki tofauti tofauti kuhusu mada ya utafiti. Aidha, imeshughulikia masuala tofauti tofauti yaliyoandikwa kuhusu jinsia katika fasihi kwa ujumla. 2.2 Yaliyoandikwa Kuhusu Mada Schermerhorn (1960) katika kitabu chake Comparative Ethic Relations: A Framework for Theory and Research, anaelezea kuwa katika mataifa yote duniani ni lazima kuwe na waliotengwa. Aidha, wanajamii ambao hutengwa sana hutoka katika makundi madogo yaliyo na hali tofauti kiutamaduni. Hata hivyo, hali hizi ni za kudhaniwa kwani zimejengwa katika akili zetu kidini, kimawazo na kijamii. Kuwepo kwa kutengwa miongoni mwa wanajamii hutegemea mabadiliko mbalimbali yanayotokea kila mara katika jamii. Kazi hii ni ya manufaa kwetu kwa sababu ilitusaidia katika kuelewa waliotengwa katika jamii hata hivyo ni utafiti tofauti kabisa na utafiti huu kwa kuwa utafiti huu umejikita katika kuangazia waliokandamizwa katika riwaya ya Maisha Kitendawili na Chozi la Heri. Senkoro (1976) ameshughulikia namna tamaduni za kikoloni na wageni ambao walikuja katika maeneo ya Afrika Mashariki hapo mwanzo katika karne ya 18 hadi mwanzo wa karne ya 19 ulivyoathiri uandishi wa kazi za kifasihi ya Kiswahili hasa riwaya. Anasema kwamba watunzi mbalimbali waliathirika pakubwa na tamaduni za kikoloni, kwa hivyo wakakandamizwa na wakoloni na hata wageni waliokuja. Ukandamizaji wa aina hii ni ule unaotokea katika kiwango cha juu zaidi kwa kuwa unatokea katika kiwango cha watunzi wa kazi za fasihi. Isitoshe, 12 anasisitiza kuwa mgogoro unaoshuhudiwa katika kazi za kifasihi hutokana na mfumo mpya wa kijamii ambao uliletwa na athari za utamaduni wa kigeni. Kazi hii ya Senkoro ilitusaidia katika kuelewa waliotengwa katika utamaduni wa wakoloni pamoja na viwango vyake. Vilevile utafiti huu umetusaidia katika kuelewa namna ambavyo watunzi wa Kiafrika wanavyoendeleza ukandamizaji huu hata baada ya uhuru kupitia kwa utunzi wao. Hata hivyo utafiti huu uliofanywa na Senkoro ni tofauti na wetu kwa kuwa utafiti huu umechunguza riwaya za Kiswahili zilizoandikwa na watunzi wa jinsia ya kike na wa kiume nchini Kenya. Mbughuni (1982) aliandika makala yanayohusu picha ya jinsia ya kike katika uandishi wa riwaya nchini Tanzania. Anasema kuwa mwanamke amesawiriwa kama mhalifu na mlaghai. Katika usawiri huu ameakisi usawiri wa mhusika ‘Hawa’ katika Bibilia kama mwakilishi wa uovu katika jamii. Mhusika huyu amesawiriwa kama mlaghai, mvuruga amani, mchoyo, mwongo n.k. Vilevile katika makala haya amemsawiri mwanamke kama mtu mwenye nafasi yake kama ya jikoni na vilevile ametawaliwa na mwanaume. Katika makala haya, mhakiki ameshughulikia usawiri wa mhusika wa jinsia ya kike na mtazamo wa mwandishi ambaye ni mwanamke kama unavyodhihirika katika kazi. Utafiti huu ni wenye utofauti na kazi tuliyofanya kwa vile yetu inaangazia namna jinsia ya kike na kiume wanavyowasawiri waliotengwa katika jamii. Kazi ya Mbughuni ni ya manufaa kwetu kwa sababu jinsia ya kike ni mwongoni mwa jinsia tunayoichunguza katika utafiti huu. Hivyo imetusaidia katika kuelewa namna ambavyo jinsia hii imekandamizwa katika jamii. Carole (1986) katika kazi yake Bad Government and Silly Literature anaelezea kuwa mwanamke au jinsia ya kike inapotambulishwa kama mtunzi tofauti basi ni kana kwamba anadunishwa. Kwake Carole, watunzi mbalimbali hufanana na hakuna yule wa jinsia ya kike au wa kiume. Hivyo 13 basi, watunzi wanapotambulishwa kwa misingi ya kijinsia basi tunamdumisha yule wa jinsia ya kike kwa kuwa watunzi ni watunzi tu. Utafiti wa Carole ni wa manufaa kwetu kwa sababu imetusaidia katika kuelewa namna ambavyo watunzi wanavyoangazia ukandamizaji katika jamii bila kuzingatia jinsia ya mtunzi huyo. Hata hivyo ni utafiti tofauti na wetu kwa sababu utafiti wetu unajikita katika vitabu au riwaya mbili za Kiswahili tofauti ambazo ni Maisha Kitendawili na Chozi la Heri. Vilevile nadharia iliyotumiwa katika utafiti huu ni tofauti na ule uliotumiwa na Carole. Chesaina (1987) kwa upande wake alichunguza umuhimu wa usawiriaji wa mhusika wa kike katika tamthilia zinazoandikwa Afrika. Anasema kuwa kuna tofauti mkubwa sana kuhusu jinsi wahusika wanawake wanavyosawiriwa na mtunzi wa kike na yule wa kiume. Kazi yake ni tofauti na utafiti huu kwa vile unajadili ukandamizaji kwa ujumla wake. Utafiti huu wa Chesaina imetuongoza katika kuhakiki namna ambavyo jinsia mbalimbali zinavyosawiriwa katika kazi za watunzi tofauti tofauti. Hata hivyo utafiti wetu umejikita katika kazi maalum za Kiswahili tofauti kabisa na utafiti wa Chesaina. Aidha, Mule (1991) alihakiki suala la wanawake katika tamthilia zilizotungwa katika Kiswahili ambazo zimeandikwa na wanawake. Alihakiki picha ya mwanamke ambayo imetokea katika tamthilia alizochagua. Anasema ya kwamba watafiti wengi ambao wameangazia suala la kusawiriwa kwa jinsia ya kike katika kazi za kifasihi wameelezea kuwa picha mbaya na ambazo zinawapotosha wasomaji wa fasihi hutokana na hoja kuwa watunzi wengi ni wa jinsia ya kiume. Anasisitiza kuwa watunzi hawa huwa wanawakilisha itikadi ambazo wanapata katika jamii ambazo wanakuzwa. Isitoshe, aliangazia iwapo kuna tofauti ya namna watunzi wa jinsia ya kiume na wale wa kike wanavyowasawiri wahusika wao katika kazi ambazo wanaziandika. 14 Utafiti huu unashughulikia vile watunzi wa jinsia ya kiume na wale wa kike katika jamii bila kutofautisha vile watunzi hawa wanavyosawiri na kuonyesha utofauti uliopo katika ukandamizaji. Utafiti huu umeonyoshe jinsi watunzi wanavyoangazia ukandamizaji. Utafiti huu ni wa manufaa mkubwa kwetu kwa kuwa umetusaidia katika kuelewa baadhi ya ukandamizaji unaowakumba jinsia mbalimbali katika jamii. Vilevile utafiti huu umewekea msingi utafiti tulioufanya. Hata hivyo, ni utafiti tofauti na uhakiki tulioufanya kwa kuwa utafiti wetu umejikita katika riwaya teule za Kiswahili ambazo ni pamoja na Maisha Kitendawili na Chozi la Heri zake Habwe na Assumpta. Isitoshe ni utafiti ambao umetumia nadharia ambayo ni tofauti na ile iliyotumiwa na Mule. Vilevile Wolf (1995) amezungumzia suala la kutengwa kwa mwanamke. Kwake Wolf, wanawake wamesawiriwa katika hali inayowafanya wamakinike zaidi ya wanaume kwani bila kufanya hivyo watakuwa na hisia ngeni kwa vile wanaakili za zinazowajali zaidi wale ambao wako karibu. Anaeleza kuwa mwanamke huegemea pande zote yaani upande wa anayenyanyasa na kunyanyaswa wakati anaandika kazi yake. Vilevile anasisitiza kuwa ni vigumu mwanamke kuwa mtunzi mkuu kwa vile hana uasili kamili kwa vile huwa wanawategemea hali ambazo zinawazunguka. Utafiti huu wa Wolf ni wenye manufaa kwa utafiti huu kwa vile umesaidia katika kuelewa namna mwanamke alivyotengwa katika jamii na visababishi vya kutengwa kwake. Pia utafiti huu umetusaidia katika kuelewa asasi mbalimbali za kijamii zinazochangia katika kutenga jinsia ya kike. Hata hivyo ni utafiti wenye utofauti na utafiti tulioufanya kwa vile utafiti wetu umeshughulikia namna ambavyo jinsia tofauti tofauti wamesawiriwa katika riwaya ya Maisha Kitendawili na Chozi la Heri. Vilevile utafiti huu umejikita katika nadharia tofauti kabasi na nadharia iliyotumiwa na Wolf. 15 Hali kadhalika Wagesa (1996) ameshughulikia namna mwanamke amekandamizwa kabla ya uhuru na baada ya uhuru barani Afrika. Anasema kuwa utatuzi kwa ukandamizaji wa mwanamke itapatikana kupitia kwa kuelimisha mwanamke kujipatia heshima na riziki au hata kujitegemea. Hivyo, watunzi wa kazi za kifasihi wanastahili kuwasawiri wanawake kama viumbe ambao wanajitegemea na walio na matumaini maishani. Utafiti uliofanywa na Wagesa ni wenye utofauti na utafiti huu kwa kuwa utafiti wa Wagesa ulijikita katika jinsia moja pekee ambayo ni jinsia ya kike. Hata hivyo ni wa manufaa kwa kuwa umetuwezesha kupata mwelekeo unaochukuliwa na wanajamii dhidi ya jinsia ya kike hasa baada ya uhuru na kabla ya uhuru. Vilevile utafiti uliofanya umeangazia jinsia mbalimbali wa umri tofauti tofauti na namna wanavyokandamizwa katika kazi za watunzi wa jinsia ya kiume na kike. Isitoshe utafiti huu umeangazia asasi mbalimbali za kijamii zinavyochangia katika ukandamizaji wa jinsia hizi tofauti. Isitoshe, Mboya (1997) ameshughulikia uumbaji upya wa mwanamke katika macho ya mtunzi Oludhe MCGoye katika riwaya Murder in Majengo, Coming’ to Birth, The Present Moment na Homing’ In. Kwa mujibu wa Mboya, mtunzi huyu anamchora jinsia ya kike kama kiumbe ambaye amepitia changamoto zilizoletwa na wanaume. Anasisitiza kuwa mwanamke anahukumiwa kihistoria inayomkandamiza na kumtenga na upangiaji wa uhuru. Aidha, mwanamke amekandamizwa na wanajamii walio na ubabedume wanaomwona kama kiumbe duni. Isitoshe, anaonekana kama anayekosa nguvu. Utafiti uliofanywa na Mboya ni tofauti na utafiti huu kwa kuwa hatulengi mwanamke pekee bali jinsi viumbe mbalimbali wanavyokandamizwa katika jamii. Utafiti huu wa Mboya umejikita katika riwaya mbalimbali lakini zilizoandikwa kwa Kiingereza na jinsia ya kike. Isitoshe ni utafiti 16 ambao umeangazia tu masuala mbalimbali anayoyapitia jinsia ya kike mikononi mwa jinsia ya kiume katika jamii. Hata hivyo ni utafiti wa manufaa kwa utafiti wetu kwa sababu tumeweza kuelewa namna ambavyo jinsia ya kiume inavyokandamiza jinsia ya kike katika jamii wanamoishi. Taasisi mbalimbali anazotumia jinsia ya kiume kumkandamiza jinsia ya kike pia zimeangaziwa na mtunzi huyu. Tunaweza kusema kuwa utafiti huu umeangazia ukandamizaji katika jicho moja bila kuangazia jamii mzima na watu wanaoishi huko. Hivyo basi utafiti wetu umechukua mwelekeo mpana mno kwa kuwa umeangazia jamii kwa ujumla wake huku ukiangazia kazi za jinsia ya kike na jinsia ya kiume na namna wanavyoangalia ukandamizaji wa jinsia zote za kijamii. Zaidi ya hayo Ogbu (1998) alishughulikia wanafunzi ambao wametengwa huku akiangazia athari mbalimbali ambazo zinaandamana na kutengwa kwake kimasomo. Alibainisha kuwa wanafunzi waliotengwa hufanya vibaya katika masomo kwa vile wamekandamizwa na wenzao. Katika utafiti huu, Ogbu amejikita katika kipengele cha elimu pekee. Utafiti huu ni wa Ogbu ni wenye faida kwa utafiti tulioufanya kwa vile umeangazia elimu kama mojawapo ya taasisi zinazotumiwa katika kumkandamiza jinsia mbalimbali za kijamii. Hata hivyo ni tofauti na utafiti tunaofanya kwa kuwa unashughulikia vipengele mbalimbali vya ukandamizaji katika jamii. Vilevile utafiti wetu umeangazia namna ambavyo watunzi wa jinsia mbalimbali wanavyoangazia ukandamizaji wa jinsia tofauti tofauti katika jamii. Vilevile ni utafiti ambao umeangazia jamii kwa ujumla wake bila kuwacha nyuma taasisi zingine. Isitoshe nadharia iliyotumika katika utafiti huu ni tofauti kabisa na ile iliyotumiwa na Ogbu. Hivyo basi ni utafiti wenye manufaa zaidi. Momanyi (1998) alichunguza vile mwanamke wa Kiislamu alivyosawiriwa katika ushairi wa Kiislamu. Alishughulikia namna mtunzi wa mashairi anavyomuumba mwanamke na sababu 17 inayomfanya amuumbe hivyo. Alihakiki tungo mbalimbali za mashairi alizoteua ili kutathmini anavyosawiriwa katika utungo huo. Utafiti wa Momanyi unasaidia katika kuelewa jinsi mwanamke wa Kiislamu anavyosawiriwa. Hivyo kupitia kwa utafiti huu tumeweza kuelewa sababu zinazochangia jinsia ya kike kusawiriwa namna au jinsi alivyosawiriwa. Hata hivyo ni utafiti ulio na utofauti na utafiti tulioufanya kwa kuwa utafiti tulioufanya unashughulikia jinsia mbalimbali za kiume na kike katika jamii. Isitoshe, utafiti huu umejikita katika dini zote za kijamii. Aidha, utafiti huu umeangazia namna ambavyo jinsia ya kike pamoja na ile ya kiume inavyoangazia ukandamizaji wa jinsia mbalimbali za kijamii. Hivyo basi ikilinganishwa na utafiti wa Momanyi, tunaweza kusema kuwa mawanda ya momanyi ni finyu tofauti na wetu. Kwa upande mwingine Zakaria (2001) katika uhakiki wake alishughulikia vile mwanamke wa Kiislamu alivyotengwa kibiashara. Zakaria alihakiki mwanamke wa Kiislamu aliyekatazwa kufanya biashara sokoni lakini anaendeleza biashara zake kisirisiri mtaani anamoishi. Alitambua kuwa mwanamke aliyenyimwa haki ya kufanya biashara hupata faida zaidi ya mwanamke huru anayefanya biashara yake hadharani sokoni. Kwa sababu wanawake wanaofanya biashara kisiri huonekana kama chombo kinachohitaji kuonewa huruma na chombo hiki hakiwezi kuleta mali mwiongoni mwa wanajamii. Utafiti wa Zakaria umeshughulikia mwanamke kutengwa kiuchumi na kidini. Utafiti huu ni wa manufaa kwetu kwa sababu umetusaidia katika kuelewa namna ambavyo mwanamke anavyotengwa kiuvhumi na kidini katika jamii. Hata hivyo ni utafiti tofauti na huu kwa kuwa utafiti huu unahusu namna waandishi wa jinsia mbalimbali wanavyozungumzia namna watu wanavyokandamizwa katika jamii katika riwaya ya Maisha Kitendawili na Chozi la Heri. Isitoshe, nadharia za tafiti hizi mbili ni tofauti. 18 Vilevile Isiaho (2001) anaeleza kuwa mwanamke amesawiriwa kuwili. Kwanza kama kiumbe mwenye kufuata maadili ya jamii yake kwa kiwango kikubwa na mwogofu na wa pili kama mtu mbaya anayechafua mazingira. Vilevile anaelezea kuwa mwanamke hashirikishwi katika shughuli za kiuchumi na zile zinazohusu jamii. Hili humfanya kutosimamia, hivyo basi ananyanyaswa na wanajamii wengine. Anatoa suluhisho la kumkomboa jinsia ya kike kwa kuwafunza watoto wasichana kuhusu namna ya kuishi katika jamii na kuitumikia. Utafiti wa Isiaho ni wenye utofauti na utafiti tulioufanya kwa vile utafiti tulioufanya umeangazia jinsi wahusika mbalimbali walivyokandamizwa kupitia kazi za watunzi wa jinsia tofauti tofauti. Vilevile tumeweza kuelewa namna ambavyo jinsia ya kike ilivyosawiriwa kama mwenye maadili na sababu zake. Isitoshe tumeweza kuelewa vigezo vinavyochangia jinsia ya kike kuharibu mazingira. Hivyo basi ni utafiti wenye manufaa kwa utafiti huu ingawa ueangazia jinsia ya kike pekee katika jamii bila kuuhusisha jinsia hizo zingine kama vile watoto na wanaume. Kimani (2003) alihakiki masuala ya kidhuluma juu ya mwanamke kama njia mojawapo ya masuala mengi ambayo yalishughulikiwa na watafiti. Alishughulikia kazi za riwaya na tamthilia. Mhakiki huyu alihakiki Rosa Mistika, Maumbile Si Huja, Mama Ee na Nguzo Mama. Mhakiki huyu alishauri utafiti zaidi ufanywe kwa kipengele cha ukandamizaji wa mwanamke kwa kuwa kuna visa vingi vya wanaume wanaodhulumiwa katika wakati wa kisasa. Anapendekeza kuwa utafiti zaidi ufanywe kuhusu kazi ambazo zimeandikwa katika wakati huu ili kuangazia namna suala hili linavyotokea. Utafiti huu umesadia katika kutambua dhuluma mbalimbali zinazowakumba wanawake katika jamii katika jamii mbalimbali. Hata hivyo ni utafiti tofauti na tulioufanya kwa kuwa utafiti huu umeangazia jinsia zote (jinsia ya kiume na jinsia ya kike). Isitoshe utafiti wetu umejikita katika riwaya mbili ambazo ni Maisha Kitendawili ya Habwe na Chozi la Heri ya 19 Assumpta. Utafiti wa Kimani ulijikita kwa tamthilia na riwaya tofauti na kazi yetu iliyojikita kwa riwaya mbili. Isitoshe Kobia (2004) anakariri kuwa kukombolewa jinsia ya kike katika jamii ya Kiafrika haupatikani bila kuuhusisha jamii yote kwa ujumla wakiwemo wanaume. Kwa mujibu wa Kobia, umoja unahitajika ili kuwakomboa jinsia ya kike pamoja na umuhimu wa ukombozi huu kwa kuwa ukombozi wake huleta uhuru wa jamii. Anasisitiza kuwa kuna umuhimu wa kumwelimisha mwanamke kwani atafunza watoto kuhusu utamaduni bora usiomdunisha mwanamke. Kwa hivyo, kumwelimisha mwanamke ni sawa na kufunza taifa lote kwa sababu msichana atakuwa mama ambaye atapata watoto na vilevile atakuwa mwalimu wa kwanza kwa hao watoto. Utafiti huu ni wenye utofauti na utafiti tulioufanya hata hivyo umetusaidia katika kuelewa namna ambavyo jinsia ya kike inavyostahili kukombolewa katika jamii kupitia kwa taasisi ya elimu. Utafiti huu haujaangazia namna ambavyo jinsia zote za kijamii zinavyoweza kujinasua kutoka katika suala hili la ukandamizaji jambo ambalo tumeliangazia kwa kifupi katika utafiti wetu. Isitoshe, utafiti wetu umezungumzia ukandamizaji wa jinsia mbalimbali na taaasisi zinazochangia katika kukandamizwa kwao kutoka kwa watunzi wa jinsia ya kiume na kike. Mwisho utafiti wetu umetumia nadharia tofauti na ile iliyotumiwa na Kobia katika utafiti wake. Wachira (2006) alichunguza picha ya jinsia ya kike na namna inavyotokea katika nyimbo za kisasa za kufoka. Alichunguza kazi za watunzi wa kike na kiume ili kuhakiki zaidi taswira ambayo anapewa mwanamke na watunzi hao ambao wanatumia mitindo ya kisasa wa rap. Aligundua kuwa msanii wa nyimbo hizi hajafaulu katika kuonyesha taswira ya mwanamke kamili ambaye anastahili kuigwa katika jamii. Utafiti wa Wachira ni muhimu katika kutuelekeza kuhusu namna jinsia ya kike inavyosawiriwa katika jamii. Hata hivyo ni utafiti tofauti na wetu kwa kuwa utafiti 20 tulioufanya unahusu vile jinsa ya kike na ile ya kiume inavyosawiriwa kama jinsia zinazokandamizwa katika jamii na watunzi tofauti tofauti. Vilevile utafiti wake ulijikita kwa nyimbo za kisasa tofauti na utafiti wetu unaojikita katika riwaya mbili za kisasa za Kiswahili ambazo ni pamoja na Maisha Kitendawili na Chozi la Heri za Habwe na Assumpta. Mwisho, Noordin (2008) ameshughulikia suala la waliotengwa huku akitumia nadharia ya kifeministi ya Kiislamu katika fasihi ya Kiswahili. Anasema kuwa jinsia ya kike katika jamii ya Kiislamu ana haki zinazolingana na za jinsia ya kiume hasa katika kipengele cha elimu inayonufaisha mtu binafsi na pia taifa. Katika kazi hii, mtunzi ameonyesha kuwa Ufeministi wa Kiislamu ulihusishwa na mwamko wa wanawake kidini kijamii na kwa msingi wa utamaduni. Nadharia hii imewezesha watu ambao wanatengwa kijinsia mwongoni mwa Waislamu na nguvu za kupata nafasi sawa na ya wanaume. Kazi hii aidha ilishughulikia hadithi fupi ya Uteuzi wa Moyoni ambayo iliandikwa na Rayya Timmammy. Utafiti huu ni wa manufaa kwa utafiti wetu hata hivyo ni utafiti uliotumia nadharia tofauti na wetu. Kazi hizi zilizoandikwa zinasaidia katika kutambua jinsi waliotengwa wanavyoonekana na jamii na namna ambavyo wanaumbwa na waandishi wa jinsia ya kiume na wa kike. Tafiti hizi vilevile zinasaidia katika kuelewa upekee wa waandishi wa kiume na wale wa kike ili kuelewa zaidi mbinu ambazo wanatumia katika kujenga ulimwengu wa kifasihi ambao wanaumba wakati wanaandika. Aidha, utafiti huu unasaidia katika kuelewa baadhi ya ukandamizaji unaopatikana katika jamii. 2.3 Hitimisho Sura hii imeweza kuangazia yaliyoandikwa kuhusu mada kwa ujumla wake. Imeshughulikia yaliyoandikwa kuhusu mada katika ushairi na riwaya. Vilevile imezungumzia yaliyoandikwa kuhusu mada hii katika fasihi ya Kiswahili. 21 SURA YA TATU MBINU ZA UTAFITI 3.0 Utangulizi Utafiti tulioufanya ulikusudia kuhakiki waandishi wa jinsia tofauti wanavyoangazia ukandamizaji wa kijamii katika riwaya za maisha kitendawili na chozi la heri. Kwa hivyo sura hii ime shughulikia mbinu mbalimbali za utafiti. Aidha maelezo mbalimbali yametolewa kuhusu muundo wa utafiti huu, wango la utafiti, usampulishaji, eneo la utafiti huu, mbinu zilizotumika katika ukusanyaji wa data ya utafiti, uchanganuzi wa data iliyokusanywa, njia za uwasilishaji wa matokeo na maadili ya utafiti yaliyozingatiwa. 3.1 Muundo wa Utafiti Utafiti huu ambao tuliufanya ulichukua muundo wa kiufafanuzi ambapo ulijikita maktabani. Data ilikusanywa kutoka vyanzo anuai hususan vitabu, majarida, makala matini na tovuti. Isitoshe, taarifa kutoka tafiti za awali kuhusiana na mada na malengo ya utafiti huu zilirejelewa kwa misingi ya kuuboresha uelewa wa kina wa suala la utafiti. 3.2 Wango la Utafiti Uhakiki wetu ulihusu waandishi wa jinsia tofauti wanavyoangazia ukandamizaji wa kijamii katika riwaya za Maisha kitendawili na Chozi la Heri. Data katika utafiti huu zilikusanywa kutokana na dondoo zilizochotwa kutoka katika riwaya mbili teule za Maisha Kitendawili na Chozi la Heri kwa misingi ya malengo ya utafiti. 22 3.3 Uteuzi wa Sampuli Utafiti huu ulitumia uteuzi wa sampuli ya kusudio. Mbinu hii ilisaidia katika kuteua riwaya ya Maisha Kitendawili na Chozi la Heri. Riwaya hizi mbili zimeandikwa na watunzi mwanamume na mwanamke ambao ni watunzi wa kazi za Kiswahili nchini Kenya. Riwaya hizi kwa kiasi kikubwa zinaangazia kukandamizwa na waliotengwa katika jamii na hata kupendekeza namna wanavyoweza kukombolewa. Riwaya hizi zimeteuliwa kwa misingi ya namna waandishi wa kazi hizi walivyowasilisha suala la ukandamizaji kwa njia ya kipekee. Isitoshe ni riwaya za karne ya ishirini na moja na zinajadili ukandamizaji kwa njia ya uwazi na undani zaidi. 3.4 Eneo la Utafiti Utafiti ambao tuliufanya ulijikita katika fasihi andishi, utanzu wa riwaya. Ulishughuilikia waandishi wa jinsia tofauti wanavyoangazia ukandamizaji wa kijamii kwa kurejelea riwaya za Maisha Kitendawili na Chozi la Heri kwa kuongozwa na malengo ya utafiti. 3.5 Ukusanyaji Data Utafiti huu ulikusanya data yake kutoka kwa riwaya ya Maisha Kitendawili na Chozi la Heri. Aidha, utafiti huu ulipata data yake kutoka mtandaoni, vitabuni, makala, maktabani na kwenye tasnifu. Ukusanyaji wa data ulifanywa kwa njia ya ukokotozi wa maandishi kutoka katika riwaya ya Maisha Kitendawili na Chozi la Heri. Utafiti ulitumia kalamu, madaftari, karatasi za kuandikia, tarakilishi na kinyonyi katika ukusanyaji wa data halikahdalika kunakilisha tuliyoyasoma kutoka kwa vitabu mbalimbali. Tarakilishi ilitumika katika kuhifadhi makala mbalimbali kutoka mitandaoni. Aidha kinyonyaji kilitumika kutoa makala kwa tarakilishi mbalimbali. 23 3.6 Uchungunuzi wa Data Data iliyochanganuliwa katika utafiti ilitoka kwa riwaya hizi mbili; Maisha Kitendawili na Chozi la Heri. Utafiti ulichanganua data hii kwa kutumia maelezo na tarakimu. Utafiti ulitumia mhimili wa nadharia ya Jinsia – Hakiki ambao ilisaidia katika kutambua upekee wa waandishi wa jinsia ya kiume na kike kuhusu jinsi wanavyowasawiri wanaokandamizwa na kutengwa katika riwaya hizi tulizochagua. Utafiti uliratibu asilimia ambayo kila riwaya inazungumzia ukandamizaji wa wahusika mbalimbali. Zaidi ya hayo, utafiti ulitumia maelezo na ufafanuzi kuwasilisha data iliyopatikana. Data hii ilisaidia kutathmini kama waandishi wa jinsia ya kiume na kike wanaangazia masuala ya ukandamizaji kwa njia sawa ama kwa njia tofauti. 3.7 Maadili ya Utafiti Kwa mujibu wa Kumar (1999), maadili ni miongoni mwa vitu vinavyopaswa kuzingatiwa katika utafiti wowote ule. Omar (2015) akimnukuu Kumar anadai kuwa vipengele vinavyopaswa kuzingatiwa katika maadili ya utafiti ni kuomba kibali, kutunza siri za taarifa kutoka kwa watafitiwa, ridhaa ya wale wanaotafatiwa pamoja na kuchukua au kupiga picha. Hata ingawa utafiti tulioufanya ulikuwa wa maktabani, suala la maadili lilitiliwa maanani katika awamu zote kuanzia kuandaliwa kwa pendekezo letu la utafiti hadi ukusanyanji wa data na uwasilishaji wa matokeo ya utafiti. Katika utafiti huu, tulihakikisha kuwa tumepata barua kutoka Chuo Kikuu cha Mount Kenya. Vilevile, tuliomba kibali cha utafiti kutoka kwa NACOSTI. Isitoshe, machapisho yote yaliyonukuliwa katika kazi hii yametambuliwa kwa kuorodheshwa kwenye marejeleo kama ilivyo ada ya kukiri vyanzo vya taarifa zetu. 24 3.8 Hitimisho Sura hii kwa ujumla imeelezea utaratibu uliozingatiwa katika utafiti huu. Maelezo kuhusu muundo unaohusika wa utafiti, wango la utafiti huu, usampulishaji, maeneo ya utafiti, mbinu mbalimbali za kukusanya data, uchanganuzi wa data iliyokusanywa, kuwasilisha matokeo na maadili ya utafiti yaliyozingatiwa. 25 SURA YA NNE UCHANGANUZI WA DATA NA UFASIRI WA MATOKEO YA UTAFITI 4.0 HISTORIA YA JOHN HABWE, ASSUMPTA MATEI NA AINA MBALIMBALI ZA UKANDAMIZAJI KATIKA MAISHA KITENDAWILI NA CHOZI LA HERI 4.1 Utangulizi Sura hii imezungumzia historia ya waandishi John Habwe, Assumpta Matei na tungo mbalimbali walizoandika kutoka miaka ya tisini (1990). Utafiti umejadili viwango vyao vya elimu na tajriba walizonazo katika uandishi wa tungo za kifasihi. Vilevile utafiti umejadili aina mbalimbali za ukandamizaji zinazoangaziwa na watunzi hawa katika kazi zao. Sura hii imeangazia tungo za Maisha Kitendawili na Chozi la Heri. Isitoshe, imeshughulikia namna ambavyo watunzi hawa wanavyokabiliana na ukandamizaji wa aina mbalimbali katika jamii zao. 4.2 Waandishi Wanaume na Wanawake Waandishi mbalimbali wa jinsia ya kiume wamejitosa katika ulingo wa fasihi ya Kiswahili. Watunzi hawa wameangazia masuala mbalimbali yanayohusu jamii yakiwemo ukandamizaji wa jinsi tofauti tofauti katika jamii. Mtunzi wa kwanza wa jinsia ya kiume wa fasihi ya Kiswahili alikuwa Fumo Liyongo aliyetunga mashairi mbalimbali kama vile Sifa la Uta, Utungo wa Ndoto au Wimbo wa Mapenzi na kadhalika katika karne ya tisa na kumi. Kwa mujibu wa Mulokozi (1996), tungo mbalimbali za Kiislamu kama vile Hamziyya (1670) na Al-Inkishafi ni kati ya tungo zilizotungwa na wanaume. Kati ya mwaka wa 1770 hadi 1840 Muyaka bin Haji alitunga tungo mbalimbali za Kiislamu. Baadaye kazi tofauti tofauti za fasihi ya Kiswahili zilitungwa na hata zingine kutafsiriwa na waandishi wa jinsia ya kiume. Watunzi hawa ni pamoja 26 na; Shaaban Robert, Mwalimu Sikujua, Abu Bakari, na watunzi wengine wengi wa kisasa kama vile Kezilahabi, John Habwe, K. W. Wamitila, Ken Walibora na kadhalika. Kwa mujibu wa Jenner (2010), watunzi wa jinsia ya kike wamekuwa wametengwa katika kutunga kazi tofauti tofauti za fasihi hasa fasihi andishi. Hata kama watunzi wachache wa jinsia ya kike ndio wameandika kazi za kifasihi, wengi wao walichipuka katika miaka ya tisini na wakati huu ndio kazi zao zilianza kuchapishwa. Mwana Kupona na Mwana Lemba (1830-1865) ni kati ya waandishi wa jinsia ya kike wa Kiswahili walio maarufu. Walikuwa watunzi wa kwanza wa jinsia ya kike waliotunga ushairi wa Kiswahili. Mwana Lemba ni mwongoni mwa waasisi wa kwanza wa fasihi ya Kiswahili. Alikulia kisiwa cha Pate na ndiye mtunzi wa Utenzi wa Siri L’Asirari katika mwaka wa 1663 utungo ulio na beti 563. Utungo huu ndio utungo wa kale zaidi katika ushairi wa Kiswahili. Naye Mwana Kupona ndiye aliyetunga Utenzi wa Mwana Kupona katika mwaka wa 1858. Kwa mujibu wa Allen (1972), utenzi huu una beti 102. Mulokozi (1999:101) anaeleza kuwa utungo huu ulitungwa na Mwana Kupona ili kumshauri bintiye Mwana Hashima katika mwaka wa 1275 baada ya Kristo. Kwake Mulokozi, utungo huu ni wa kitamaduni na kimawaidha katika kipindi kile. Kwa sasa watunzi wengine wa jinsia ya kike wamejitokeza na wameandika tamthilia, riwaya, hadithi fupi na mashairi. Watunzi hawa ni pamoja na; Pauline Kea, Rayya Timammy, Assumpta Matei, Peninah Muhando na Clara Momanyi 4.3 Historia ya John Habwe John Habwe kwa sasa ni profesa na tena mhadhiri wa Kiswahili kwa zaidi ya miaka 30 katika Chuo Kikuu cha Nairobi nchini Kenya. Mwandishi huyu alizaliwa mnamo mwaka wa elfu moja mia tisa sitini na mbili (1962) kule Emuhaya ulioko Mkoani mwa Magharibi na huko ndiko 27 alikokulia. Alipata elimu yake ya msingi katika shule ya Ebukhaya huku ya sekondari akipata katika shule ya Ebwali alikosomea kidato chake cha kwanza hadi cha nne. Baada ya masomo haya aliyoyapita, alijiunga na shule ya sekondari ya Kaptet ambayo kwa sasa inajulikana kama shule ya sekondari ya Tengecha. Katika shule hii aliyaendeleza masomo yake ya kidato cha tano na sita. Katika kipindi hiki cha masomo ya sendondari ndipo alipoanza kuimarika na kuipenda masomo ya Kiswahili. Suala hili lilimpelekea kusoma majarida, magazeti na vitabu vingi vilivyoandikwa kwa Kiswahili kama hatua za kujiendeleza katika somo hili. Walimu wake walimsaidia kukuza somo hili na hata kumhamasisha baada ya kubaini mapenzi yake katika somo la Kiswahili. Baada ya masomo ya sekondari, Habwe alipita na kujiunga Chuo Kikuu cha Nairobi. Chuoni alisomea Kiswahili na kuhitimu na shahada ya B.A katika Kiswahili mnamo mwaka wa 1984. Aliendeleza masomo yake ya uzamili na kuhitimu katika mwaka wa 1988 na shahada ya Uzamili katika somo la Kiswahili. Utafiti alioufanya wakati huu ulihusu Amali Mtagusano wa maana na Jamii ya Wamvita. Aliajiriwa na kufundisha somo la Kiswahili kwa muda katika chuo hicho kuanzia mwaka wa 1995 hadi mwaka wa 1999 huku akiendelea na Shahada yake ya Uzamifu katika Isimu. Anatajriba na uzoefu mkubwa katika Sarufi na Fasihi ya Kiswahili. Mwandishi Habwe anaelezea kuwa alipata athari kubwa kutoka kwa wahadhiri na walimu wake ambao ni pamoja na Profesa Mohammed Bakari, Profesa Mohammed H. Abdulaziz ambao walikuwa wahadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Isitoshe, aliathiriwa na Profesa Jay Kitsao na Bwanna Kadenge ambao kwa sasa ni marehemu. Anasisitiza kuwa mengi anayoyafanya ni kama walivyokuwa wanafanya. Utunzi wake umepata athari mkubwa kutoka kwa kazi za waandishi maarufu Leo Toistory na Profesa Euphrase Kezilahabi ambao wanaondoka Ughaibuni na Afrika Mashariki. Kazi zao 28 zilianza kumvutia tangu akiwa mwanafunzi na hadi wa leo haujakoma kumvutia. Anaelezea kuwa wao ni watunzi mashupavu na tena watajika wa sanaa kubilizi. Kila wakati anapotunga yeye hulenga kuvifikia viwango vyao au hata kuvipita. Profesa Habwe alikuwa mwenyekiti wa Idara ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Nairobi kuanzia mwaka wa 2013 hadi 2016. Isitoshe, alikuwa mwenyekiti wa Idara ya Isimu na Lugha kwa miaka miwili katika chuo hicho. Vilevile ni mshauri wa mashirika mbalimbali yanayochapisha vitabu na taasisi mbalimbali za masomo nchini Kenya. Profesa Habwe ni mshauri wa watunzi wanaobuni kazi za kinadhari na watafiti wa vyuoni. Aidha, amewahi kuwa mhadhiri wa muda katika Chuo Kikuu cha Moi, Maseno na Catholic. Zaidi ya hayo amewahi kufanya kazi na mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserekeli kama vile Umoja wa Mataifa, Shirika la Afya Duniani na Kamati ya tafsiri ya Afrika Mashariki. Kwa muda mrefu amekuwa mwenyekiti wa kipindi cha Lugha yetu na Mjadala katika radio ya Kenya Broadcasting Corporation (KBC). Profesa John Habwe ameshiriki katika utafiti na uandishi wa kazi nyingi za kifasihi, Isimu na isimu jamii. Baadhi ya kazi alizoziandika ni pamoja na: Hidaya (2018), Shujaa wa Taifa (2017), Hadaa la Nafsi (2014), Kovu Moyoni (2014), Pendo la Karaha (2014), Lulu ya Maisha (2013), Mikono ya Gondi (2012), Pamba (2011), Fumbo la Maisha (2011), Safari ya Lamu (2011), Siku ya Kheri katika Mwavyaji Roho na Hadithi Nyingine (2011), Ungamo la Janaha (2010), Uchochoro wa Mauti katika Mizungu ya Manabii na Hadithi Nyingine (2010), Mbunge katika Mizungu ya Manabii na Hadithi Nyingine (2010), Fumbo la Maisha (2009), Cheche za Moto (2008), Cheche za Moto (2008), Sofia Mzimuni (2008), Maisha Kitendawili (2007), Kasheshe la Mji katika Mimba Ingali Mimba (2006), Paradiso (2005), Mkimbizi katika Mayai Waziri wa Maradhi (2004), 29 Walicheka Kicheko katika diwani ya Mwenda Wazimu na Hadithi Nyingine (2000) na Maumbile si Huja (1995). Tungo hizi zinaangazia nyanja mbalimbali za maisha ya wanajamii hasa usawiri wa jinsia tofauti tofauti na ukandamizaji wa jinsia hizi katika jamii. John Habwe ni mmoja kati ya waandishi wa kiume walioweza kuandika kazi kadha kuhusu nafasi ya jinsia mbalimbali katika jamii. Tumetumia utungo wa Maisha Kitendawili (2007) ili kuangazia mtazamo wa mwandishi huyu kuhusu jinsia anavyowashughulikia jinsia tofauti tofauti wanaokandamizwa katika jamii. 4.4 Historia ya Assumpta Matei Assumpta sasa hivi ni daktari na afisa mkuu wa mtihani katika baraza kuu la mtihani nchini Kenya. Assumpta Matei ni mwandishi na mwalimu mwenye uzoefu mkubwa katika kufundisha lugha na fasihi ya Kiswahili katika vyuo vikuu na shule za sekondari nchini Kenya. Kati ya taasisi alizowahi kufundisha nipamoja na; Catholic University of East Africa na shule ya wasichana ya Kenya High. Aidha, ameshiriki katika majopo mbalimbali ya kukuza, kutekeleza na kutathmini mitaala ya elimu nchini Kenya. Baadhi ya kazi alizoziandika ni pamoja na; Kurunzi ya Kiswahili: Kitabu cha Mwanafuzi (2018), Chozi la Heri (2017), Darubini ya Isimujamii: Ufafanuzi Kamili wa Sarufi ya Kiswahili: Maswali na Mazoezi (2014) na Fani ya FasihiSimulizi kwa Shule za Upili (2011). Kazi hizi za Assumpta zimeangazia nyanja tofauti tofauti kuhusu maisha ya wanajamii hasa ukandamizaji wa jinsia mbalimbali katika jamii. Mtunzi huyu ni mmoja kati ya watunzi wa kike walioweza kuandika kazi mbalimbali kuhusu nafasi ya jinsia tofauti tofauti katika jamii. Tumetumia riwaya ya Chozi la Heri (2017) ili kuhakiki mtazamo wake katika kuangazia jinsia mbalimbali wanaokandamizwa katika jamii. 30 4.5 Muhtasari wa Riwaya ya Chozi la Heri Riwaya ya Chozi la Heri ni kazi ya fasihi andishi iliyoandikwa na Assumpta K. Matei. Riwaya hii ni kazi inayoangazia tamaa kubwa inayotokea ambayo inahusu kumiliki nyenzo mbalimbali za wanajamii za kujiinua kisiasa na kiuchumi. Tamaa hii inachangia katika kusambaratika katika asazi mbalimbali za kijamii na hata muundomsingi wa mshikamano wa wanajamii. Maazimio ya wanajamii ambayo wanashindwa kuafikia yanachangia katika kuzua hali ya kuvunjikiwa kwa wanajamii hawa hasa kiroho. Hata hivyo, baada ya kazi nzito wanaoshiriki wanajamii, kunatokea jamii mpya iliyo na watu wenye matumaini na usawa wa hali ya juu. 4.6 Muhtasari wa Riwaya ya Maisha Kitendawili Riwaya ya Maisha Kitendawili ni fasihi andishi ambayo imeandikwa kwa lugha ya mguso na mnato na John Habwe. Riwaya hii inashughulikia machafuko ya kisiasa inayotokea katika jamii baada ya matabaka mbalimbali ya kijamii kushiriki katika ugomvi. Vilevile riwaya hii kwa kiasi kikubwa imeangazia masuala ya usasa na ukale. Isitoshe, riwaya hii imeangazia masuala ya mahaba yanayotokea chuoni wakati wanafunzi wanapoendeleza masomo yao. Zaidi ya hayo, kutokana na masuala haya ya machafuko ya kighasia na elimu, jamii inafikia mwamko mpya ambapo matabaka mbalimbali wanaonekana kuwa wenye usawa na furaha mwingi. Isitoshe jamii hii inakuwa yenye matumaini na amani. 31 4.7 Aina Mbalimbali za Ukandamizaji wa Jinsia Tofauti Tofauti katika Riwaya ya Maisha Kitendawili na Chozi la Heri 4.7.1 Utangulizi White na Couzens (1984:148) anasema kuwa watunzi ni wanajamii wanaotoka katika jumuiya maalum. Kama wanajamii, basi wanatarajiwa kueleza kwa njia ya wazi malalamiko na matatizo ya watu wao. Vilevile wanatarajiwa kuweka wazi matamanio walionayo ambayo ni ya pamoja. Waandishi wa fasihi ya Kiswahili ndio macho ya jamii mbalimbali. Wasanii hawa hutoa taswira kamili ya migogoro ama mafanikio yanayoyakumba jamii yao katika maisha ya kila siku. Watunzi mbalimbali wa fasihi ya Kiswahili wameangazia masuala ya ukandamizaji wa jinsia tofauti tofauti katika kazi zao. Suala hili lina ukweli ambao haupingiki kwa vile tunayashuhudia katika uhalisi wa maisha yetu ya kila siku. Kwa kutumia Nadharia ya Hakiki – Jinsia, ukandamizaji wa jinsia tofauti tofauti unatokea kwa njia ya wazi. Suala hili linatokana na itikadi, desturi, historia na mila za jamii za Kiafrika. Katika sura hii, tunaangazia aina mbalimbali za ukandamizaji wanazozipitia jinsia mbalimbali katika riwaya teule za Kiswahili. Aidha, tunajadili sababu ambazo zinaleta hali hii ya ukandamizaji wa jinsia tofauti tofauti. 4.7.1.1 Ukandamizaji wa Kijinsia katika Chozi la Heri Kuna ukandamizaji wa aina mbalimbali katika riwaya ya Chozi la Heri. Ukandamizaji huu ni pamoja na: 32 4.7.1.2 Vifo, Misiba, Mauaji na Majonzi Jinsia tofauti tofauti hukabiliwa na ukandamizaji wa kuuawa na viongozi, wanasiasa, wanaume na hata wanawake wengine. Mauaji haya yanatokana mara nyingi na yale majukumu jinsia mbalimbali wamepewa na jamii kama vile walinda familia, wakombozi, watetezi wa jamii, watega uchumi na walinzi wa jamii. Majukumu haya yanafunzwa kwa jinsia mbalimbali kutoka wakiwa wachanga hadi wanapokuwa wazima na hata kupewa majukumu katika jamii. Katika riwaya ya Assumpta Chozi la Heri (2017), tunamkuta mhusika daktari Ridhaa akiwa amezidiwa na majonzi makubwa ambayo yanatokana na misiba mikubwa ambayo imemkumba. Jumba la Ridhaa la kifahari limeteketea moto huku watu wa jamii yake wakiungua humo. Katika mikasa hii, mkewe Terry pamoja na wanawe wawili Tila na Mukeni. Jumba la daktari Ridhaa liliungua moto lote kukabaki tu kiunzi na majivu na mashizi. Mtunzi anaeleza kuwa hakuna kilichookolewa. Ridhaa alisimama kwa maumivu makali, mikono kairudisha nyuma ya mgongo wake uliopinda kwa uchungu. Macho yake yaliyotanda ukungu alikuwa kayatunga juu angani, akitazama wingu la moshi lililojikokota kwa kedi na mbwembwe; wingu lililomnywesha na kumkumbusha ukiwa aliozaliwa nao na ambao alihofia kuwa angeishi na kuzikwa kwao. Mara aligeuka, akawa anatazamana ana kwa ana na tunari la moto ambalo lilikuwa linaliteketeza jumba lake la kifahari huku likimfanyia tadi kana kwamba linamhakikishia kuangamia tena kwa nguvu zake. (Uk.1) Zaidi ya haya, tunaarifiwa kuwa Daktari Ridhaa alikuwa amepoteza majumba yake ya biashara kwa moto na pia kwa ubomozi wa kimaksudi kutoa nafasi kwa ujenzi wa barabara. Katika riwaya hii, mtunzi anaeleza kuwa Bw. Ridhaa ambaye alikuwa tajiri mkubwa wa kusifiwa amekuwa maskini kighafla. Tunaelezwa kuwa jamii ya Ridhaa ilikuwa imepatwa na msiba hapo awali wakati walipompoteza mwanao Dedan Kimathi aliyekuwa kitindamimba. Misiba hii, hasa ya hivi karibuni inayompiga Ridhaa mtawaliwa inamnyong’onyeza mwili na kumyeyusha matumaini yote 33 na anabaki kama kaka tupu. Misiba hii inayotokea mwanzoni mwa riwaya hii inatufanya sisi kama wasomi kujihisi kikamilifu na mhusika Ridhaa kwa njia ya huruma na kutukuzia shauku ya kufuatilia kisa chote ili tupate kufahamu hatima ya yote yaliyojiri baadaye. Fauka ya haya, msiba mwingine unaomwandama Ridhaa na hata kumwongezea simanzi zaidi unatokana na kukimbilia msitu wa Mto Mamba baada ya ghasia ambazo zinazuka baada ya uchaguzi mkuu nchini Uhafidhina. Ridhaa na familia zingine wanahamia msitu ulio katika sehemu ya mbali wanakolazimika kuanzisha makazi mapya yaliyo duni pamoja na shida zingine zinazoambatana na hali yao ya ukimbizi. Wanasakarika kwa njaa na ukosefu wa maji safi mbali na kutamauka. Jambo hili linatufanya tuzidi kumhurumia Ridhaa na wakimbizi wenzake pamoja na kutuangazia ushupavu wa Ridhaa wa kukabiliana na mikosi ya kidunia. Tunavutiwa katika kutamani uvumilivu wake na wenzake walio naye. Riwaya hii imejaa mifano tele ya mikasa inayotibua majonzi makuu nyoyoni mwa watu. 4.7.1.3 Changamoto za Vijana Katika kazi hii, tunatumia neno vijana ili kurejelea watu waliopita umri wa utoto lakini hawajakomaa kiumri. Neno hili linasimamia vikundi viwili vya watu wa jinsia tofauti ndani yake. Hivyo, inawauhusisha wasichana na wavulana. Katika riwaya ya Chozi la Heri, vijana mbalimbali wamesawiriwa kama watu wanaopitia ama wanaokumbwa na changamoto tofauti tofauti kutegemea uana na jinsia yao. Vilevile kuna changamoto ambazo zinawakumba vijana wote kwa ujumla. Baadhi ya changamoto za kijumla zinazowakumba vijana ni pamoja na ukosefu wa ajira. Msimulizi katika ukurasa wa 21-24 anaelezea kuwa vijana wanapomaliza kusoma, wanakosa ajira na ile ambayo ipo aghalabu hutolewa kwa njia ya mapendeleo na kama huna mhisani basi pia huna 34 njia ya kupata ajira. Vilevile vijana wengi wanashauriwa ili waanzishe biashara zao wenyewe ili kujikimu ilhali hawana mtaji wa kuanzisha hizo biashara wala hawajapewa stadi kamili katika zile biashara huko masomoni. Hivyo, vijana wanabaki katika mtanziko. Wakati mwingine vijana hushauriwa kurudi mashambani kutoka mijini ilhali yale mashamba yanamilikiwa na matajiri ama walowezi kutoka nchi za nje ambao utawala unadai kuwa wanasaidiwa kuendeleza nchi ilhali ukweli ni kwamba wanainyonya nchi na kuwanyima wazawa nafasi za kutumia hiyo arthi. Jambo hili linafanya vijana kubaki maingainga pasipo cha kutegemea. Mja huyu alikuwa kavaa shati lililoandikwa ‘Hitman’ mgongoni. “Nyamaza wewe! Nyinyi ndio mliturudisha nyuma miaka yote hii. Mnatuhadaa kwa vishahada mnavyotupa vyuoni, vishahada ambavyo ni laana kwetu, tunuri hasa linalouchoma uwepo wetu. Mnatufunza kukariri nadharia bila kuwazia umuhimu wa kutupa umilisi na stadi za kutuwezesha kujitegemea na kuyadhibiti maisha yetu ya baadaye. Mtu anahitimu hata digirii tatu, kisha anapiga lami kwa miaka kumi bila kuwaza kuwa anaweza hata kujiajiri. Najua unaniona kuwa asiye na akili. Hata hivyo, hebu niambie, mtu ataweza vipi kujiajiri na hata njuga zenyewe za ujasirimali hajafungiwa chuoni? Isitoshe, hata wanaoweza kupapatisha huo ujasirimali watatoa wapi mtaji wa kuanzishia biashara? Wapo viongozi wanaopita wakipayuka, ‘Vijana turudini mashambani. Maeneogatuzi yenu yanahitaji mabarobaro kama nyinyi kulisukuma gurudumu la maendeleo.’ Hapa ndipo unashangaa utarudi kwenye shamba lipi na tangu hapo familia yako uliiacha ikiishi kwa msaada wa wale wale waliotoka mbali kule walikotoka, wakapewa maelfu kwa maelfu ya ekari, wakajenga viwanda na maduka ya biashara, wengine wakalima mashamba makubwamakubwa huku wakidai kuwa ni njia ya kuwahakikishia wenyeji hali ya kujitosheleza kwa chakula…” (Uk 21-22). Vilevile vijana wamesawiriwa kama watu wanaopitia changamoto mbalimbali kama vile kutumiwa kwa vijana na wanasiasa mashuhuri kuzua ghasia ambazo zinawanufaisha hao matajiri waliomamlakani. Kwa mfano; ghasia za baada ya uchaguzi nchini Uhafidhina zinapoanza, vijana ndio wanaotumiwa kuzusha na kueneza vurugu, kuimba nyimbo za uchochezi, kubeba mabango katika maandamano, kutetea matajiri wanyanyasaji na hata kuchoma mali. Isitoshe, vijana wanakumbana na makali ya vyombo vya dola kama vile jeshi la polisi ambalo linawaangamiza kama inavyoelezwa katika kisa cha kusai amri (Uk. 24-25). 35 Baadaye ving’ora vilisikika kwa mbali. Yale malori ya kawaida yanayobeba askari almaarufu katika janibu hizi, ‘Penda Usugu Ujute’, yakaonekana yakielekeza mianzi ya pua karibu na walipokuwa vijana hawa, vitoza machozi vikahanikiza hewa ya asubuhi, polisi wakawa wanawawinga mabarobaro hawa kama kengewa wala vifaranga au ndege wala nafaka. Hata hivyo, mabarobaro hawa walioonekana kuwa na kasasi na maisha walikita ardhini kama mikuki iliyochomekwa hapo. “Hatung’atuki,” walisema huku wameinua mikono yao juu. Baada ya muda mfupi vifua vyao vilikabiliana na risasi zilizorashiwa vifua hivyo kama marashi, vifua vikawa havina uwezo dhidi ya shaba, vijana wakaanguka mmoja baada ya mwingine, wamekufa kifo cha kishujaa, wamejitolea mhanga kupigania ‘Uhuru wa Dhati’, kama walivyouita. Machozi yalinitiririka bila kuzuia. Niliwahurumia vijana hawa wakembe ambao walikufa kifo walichoweza kukiepuka. Niliihurumia nchi yangu ambayo ilielekea kushindwa kuwashawishi watu wake kutambua umuhimu wa usalama (Uk 24-25). Zaidi ya hayo, vijana wa kiume wametumiwa kulangua dawa za kulevya. Kwa mfano; Dick katika uk wa 120 anatumiwa na Bw. Buda kusafirisha na kueneza hizi dawa. Vijana wanalazimika kufanya hivyo kwa sababu ya kutekwa bakunja kama alivyo Dick ama wamepigwa na uromo au umaskini mpaka hawana namna nyingine ya kuishi. Mfano katika riwaya: “…Dick amesafirisha maelfu kwa maelfu ya vifurushi vya dawa hizi. Mwanzoni hakuwa mraibu wa dawa hizi lakini ilibidi ajizoeshe, kwa usalama wake mwenyewe, kwani mara nyingi ilibidi kuzimeza dawa zenyewe ili kwenda kuzitapika kwenye masoko ughaibuni. Hili lilitokea wakati mashine za forodhani zilipopata makali zaidi siku nyingine na kung’amua shehena ambazo zilikuwa zimeshonewa vibindoni!” (uk 120). Isitoshe, vijana wa kike nao wamesawiriwa kama watu wenye changamoto zao za kipekee kama vile kubakwa namna kijakazi Sauna anavyofanyiwa na babake wa kambo Maya katika ukurasa wa 145 – 147. Naye msichana Zohali anapata uja uzito kama angali shuleni na hali ya unyanyapaa inamfika akiwa kwao inayomlazimisha kugura kwao na kuanza kutamba na dunia (Ukurasa wa 98 – 101). Zohali aliendelea, ‘Maisha yangu yalianza kwenda tenge nilipojiunga na kidato cha pili. Unajua hali ya mtafaruku wa kuhisia inayowapata vijana katika umri huu. Niliikumbatia hali hii kwa papara za ujana, kutahamaki nikajipata nimeambulia ujauzito. Naikumbuka vizuri sauti ya mwalimu mkuu wakati alipotoa hukumu ya kifo. 36 “Dadake Zohali, samahani sana lakini uchunguzi unabainisha kwamba Zohali ni mjamzito. Nimekuita hapa ili uweze kumrejesha nyumbani. Akijifungua wazazi wake wanaweza kumtafutia shule nyingine,” Zohali aliingiza sauti nzito ya mwalimu mkuu. Kwa upande mwingine Mwanaheri anakumbwa na tatizo la kutengana kwa wazazi wake suala linalomfanya akose mtu wa kutegemea. Vijana wengi katika riwaya hii pamoja na watoto wanatatizo kubwa la kutokuwa na walezi wanapokuwa hawajafikia wakati wa kujitegemea. Mifano ni kama Umu, Dick, Mwaliko, Cynthia na kadhalika. Almuradi kuna changamoto tele za vijana katika riwaya hii ambazo suluhisho angalabu huwa kudura za Mwenyezi Mungu (Uk. 93- 98). “Nasikia mama yangu ametoka kwenye jamii ya Bamwezi, baba mnajua jamii yake bila shaka. Daima mama alichukuliwa kama mgeni, si katika boma let utu, bali pia katika kijiji kizima. Haikuwa ibra kumsikia nyanya akimrejelea mama kama Muki, yaani ‘Huyo wa kuja’, na kusema kwamba msichana Bamwezi, hata akiwa na umri wa miaka tisini ni msichana wa Bamwezi tu. Haya yalilengwa kumkumbusha kwamba yeye hakuwa wetu. Uhasama ulizidi baada ya vurugu za miaka mitano iliyopita. Nyanya alimwona mama kuwa chanzo cha kuharibiwa kwa mali yetu, kwamba ndiye aliyewafanya majirani zetu kutuchomea boma ili watuondolee gugu ambalo liliutia najisi utambulisho wetu. Nilimtazama mama akidhoofika kiafya kwa majonzi ya kutengwa na wale aliowadhania ni aila yake. Sikujua kilichokuwa kinamdhili siku hizo, ila nilisikia kuwa mlikuwa na mvutano kati yake, baba na nyanya. Mwanaheri alisafisha koo na kuendelea kwa sauti iliyolemaa. “Jahazi letu liligonga mwamba asubuhi moja nilipoamka na kupata kibarua juu ya meza ndogo iliyokuwa chumbani mwangu…” (uk. 94 – 95). 4.7.1.4 Ukabila na Ubaguzi Suala la ukabila hurejelea mwenendo wa kutenga na mapendeleo unaoonyeshwa watu na ukoo fulani huku watu wengine wakipuuzwa. Kwa upande mwingine ubaguzi ni kitendo cha kuwapendelea kikundi fulani cha watu na kuchukiwa kwa wengine wasio wa kikundi hicho. Suala la ukabila na ubaguzi ni suala linalosawiriwa katika riwaya hii kupitia kwa wahusika mbalimbali. Misingi ya matukio mengi katika riwaya hii ni ukabila na ubaguzi. Kwa mfano, Ridhaa na familia yao wanapoletwa na baba yao kuishi katika eneo la Msitu wa Heri, wanapokelewa huko na kupewa 37 lakabu ya Wafuatao Mvua kwa maana ya waliohamia huko kwa ajili ya ukosefu wa mashamba kwao. Lakabu hii inatumiwa kuwatenganisha na wananchi ambao ni wazawa wa eneo la Msitu wa Heri. Ridhaa anapokuwa shuleni anabainisha kuwa wanafunzi wenzake wanambagua kwa mujibu wa kabila lake kwa kumwita Mfuata Mvua. Masomo ya Ridhaa mwanzoni yanatatizika kidogo kwa hali hii lakini kwa bahati nzuri anapitia hiki kizingiti na kufaulu katika masomo. Ridhaa hakuwa mkazi asilia wa Msitu wa Heri. Alikuwa ‘Mfuata Mvua’ kama walivyoitwa walowezi na wenyeji kindakindaki. Hakupachagua mahali hapa, majaliwa yalitaka, na majaliwa yana nguvu! Baba yake yasemekana alikuwa na wake kumi na wawili. Unajua zama hizo hali ilivyokuwa! Mzee mwenye wake na wana wengi alihesabiwa kuwa mkwasi kwelikweli. Basi wake hawa hawakuchelea kutimiza amri ya maumbile, wakapania kuujaza ulimwengu! Ardhi ya Mzee Mwimo Msubili ikawa haitoshi kuyalelea madume yake ishirini. Iligawanywa hadi ikawa vikataa, ikalimwa na kupaliliwa mpaka ikachoka. Hatimaye Mzee Mwimo Msubili alijiona amekabiliwa na kibarua kigumu cha kuvilisha vinywa hivi kutokana na zao dogo alilolipata (uk 8). Mikasa ya kuchomeka kwa kasri la Bw. Ridhaa inahusiana na ukabila na ubaguzi, ni kama yeye na wengine wasio wa eneo hili wanalengwa kuangamizwa. Mchafuko unapozuka baada ya uchaguzi, watu kama vile Ridhaa, ndugu Kaizari, Selume, Kiriri na Kangata wanalazimishwa kuhama makazi yao na kukimbilia Msitu wa Mto Mamba na baadhi yao kuanzisha huko makazi mapya. Wanatimuliwa kutoka makazi yao na ‘Wafuata Mvua’. Hali hii inatatiza mshikamano na utulivu wa taifa. Kuyumba kwa taifa kunaletea raia shida nyingi mno zinazokwamiza kukua kwa taifa. Vilevile mtunzi amewasawiri jinsia mbalimbali kama watu wanaopitia ubaguzi tofauti tofauti. Suala hili linadhihirika kwa uwazi zaidi wakati wa uchaguzi ambapo mgombeaji wa kike Bi. Mwekevu Tendakazi anaishia kushinda dhidi ya mpinzani wake wa kiume Bw. Mwanzi. Jambo 38 hili linaleta mtafaruku mkubwa katika nchi kwa vile wanaume wengi hawakubali kuwa wanaweza kuongozwa na mwanamke japo amechaguliwa kihalali (uk 16-17). Kwa mfano: Siku ile baada ya kutawazwa kwa kiongozi mpya, mbingu zilishuka. Misukosuko inayoikumba nchi ya Uhafidhina na kuiletea maangamivu makubwa inatokana na ubaguzi wa kijinsia; kuna imani kuwa ni mwanamume tu anayeweza kuitawala nchi. Hii ni imani potovu kwa vile haina misingi ya kidemokrasia wala mantiki. Mtunzi vilevile amezungumzia suala la ubaguzi wa kitabaka pale ambapo Kimondo anamwambia Lunga na wanafunzi wenzake kuhusu namna kulivyoenea ubaguzi katika asasi za kiafya ambapo mgonjwa hawezi kutibiwa kwa sababu hayumo katika tapo la watu wenye stahiki ya kutibiwa katika kituo maalumu. Kimondo anatupa kauli ya daktari akimshauri muuguzi. “Daktari, Mwafrika mwenzako, anakukazia macho na kumwambia muuguzi, His father is a casual labourer. We cannot treat him. The company does not have any medical scheme for casual labourers. Muuguzi anayasikiliza maneno haya, na baadaye kuwa mkalimani wako, anadhani huelewi lugha hii. Sijui, Lunga, kama umewahi kujiuliza kama huduma bora za afya zinastahili tu kwa watoto wa walio nacho. Je, mwana wa kibarua, ambaye ndiye anayezalisha mali ya kuwezesha kuwepo kwa hiyo medical scheme, hastahili kupewa huduma ya matibabu? Naona umekuwa ukuni kwenye uchaga, unaoucheka ulio motoni,” Kimondo angekamilisha uzungumzi wake na kujipangusa matone ya jasho ambayo yangekuwa yametunga kipajani mwake bila kujali mtazamo wa wenzake ambao wangekuwa wanaisikiliza hotuba ya Lunga (uk 70). Katika mfano huu, mgonjwa anabaguliwa kitabaka, hawezi kupata matibabu kwa sababu kazi anayoifanya katika kampuni haiwezi kumpa bima ya kutosha ya kimatibabu. Isitoshe, mtunzi ameangazia tofauti baina ya Bw. Ridhaa anayeishi katika mtaa wa Afueni na mlevi Shamsi aishie katika mtaa wa Kazikeni ambao unaletwa na suala la utabaka ambapo Ridhaa anaonyeshwa kama tajiri huku Shamsi akisawiriwa kama maskini. Ridhaa anamtazama Shamsi akipita hapa kama afanyavyo kila siku. Mtaa anakoishi Shamsi si mbali na hapa, unaweza kusema Shamsi na Ridhaa ni majirani. Hili la kuwa jirani wa Shamsi limetokea baada ya miezi mingi ya fikira na tafakuri. Kwa kweli huu ni mwezi wa tatu tangu Ridhaa kuhamia kwenye mtaa wa Afueni. Afueni ni mtaa wa raia wenye kima cha juu kiuchumi. Mtu anapoutazama mtaa huu husalimiwa na majengo ya 39 kifahari ya ghorofa, yale ambayo yanaitwa katika janibu hizi ‘town houses’. Daraja kubwa limeutenga mtaa huu na mtaa wa Kazikeni ambako ndiko familia ya Shamsi na nyingine za aina yake zinakoishi. La! Haziishi, zinaambulia maisha ya kubahatisha tu. Ni mtaa wenye mabanda athari yaliyojengwa kwa udongo na mabati (uk 137-138). 4.7.1.5 Masuala ya Ghasia Ghasia ni visa au kisa kinachoenda kinyume na utulivu na amani katika jamii. Hivyo ni mchafuko na vurumai katika jamii. Katika riwaya ya Chozi la Heri, wahusika wenye jinsia mbalimbali wanasawiriwa kama watu wanaoendeleza ghasia kadhaa wa kadhaa. Kwa mfano, baada ya uchaguzi ambao unashindwa na mgombezi wa uongozi Mwekevu Tendakazi, tunashuhudia visa vingi vya vurumai vinavyotibua amani na utulivu. Msimulizi anatuelezea yafuatayo; Kilichofuatia maneno haya (matangazo katika runinga) kilisikitisha. Niliwaona mabarobaro wamebeba mabango yaliyochorwa picha za mpinzani wa kiume ambaye alishindwa na Mwekevu katika uchaguzi. Wote walikuwa wakighani mkarara huu: Tawala Wahifidhina tawala, Mwanzi wetu tawala Wahifidhina tawala Mara hali ilibadilika, nikaona wote wameyazingira magari barabarani na kuanza kuyawasha moto kana kwamba wanayachoma mabiwi ya taka! Baadaye kulisikika vilio vya imani, binadamu akiomba kuhurumiwa na binadamu kaini, vilio ambavyo viliangukia masikio yaliyotiwa nta. Magari yaliwaka moto bila kujali kilichomo ndani. Moshi ulipaa mbinguni katika mstari mmoja kama kwamba unakwenda kumshtakia Mungu (uk 20). Mtunzi anaeleza kuwa vijana wanajitosa katika visa vya ghasia na utovu wa nidhamu ambapo wanachoma magari, wanapora maduka na hata kuwapiga watu. Nao polisi wanapofika kuna kuwa na umwagikaji wa damu. Ukosefu wa amani ambao unaletwa na vitendo vya ghasia vinavyoletwa na jinsia tofauti tofauti unasababisha maafa mengi, unaleta kusimama kwa biashara, unaharibu uhusiano baina ya majirani na marafiki, unasababisha watu kutoroka katika majumba yao huku wengine wakiuliwa. Vilevile jambo hili linasababisha vitendo vingine vya tandabelua na utovu wa amani. Zaidi ya hayo, kwa sababu ya ghasia mhusika kama vile Ridhaa na wenzake wanatorokea Msitu wa Mamba ili wajinusuru maana nchi yao haitawaliki. 40 Suala la ghasia vilevile linaendelezwa katika eneo la Msitu wa Mto Mamba wanakoishi wakimbizi. Baada ya wakimbizi kutamakani huko kwa kipindi fulani, kunazuka mtafaruku wa kitabaka baina ya wakimbizi mpaka jamii hii inasambaratika na kuguria kwingine. Visa hivi vya ghasia na ukosefu wa utulivu miongoni mwa wakimbizi vinatibua amani na kusababisha mtawanyiko wa watu (uk 74-77). Polepole uhasama ulianza kutishia kuisambaratisha jamii ya Msitu wa Mamba. Viongozi, kwa kuhofia kovu kuwa jeraha, walianza kampeni za kuwaelimisha raia kuhusu umuhimu wa kuishi kwa amani licha ya tofauti zao za kiusuli. Hata hivyo, hizi zilikuwa juhudi za mfa maji. Awamu ya kwanza ya vita vya wenyewe kwa wenyewe ilianza; walinda usalama walitumwa kukabiliana na mgogoro huo. Busara yao ya kuwasaka wahalifu kwa mitutu ya bunduki iliwaacha wengi wakiwa wafu, watoto wakabaki wanawasaka. Isitoshe, suala la ghasia limeshughulikiwa mwanzoni mwa riwaya hii wakati jamaa, familia na mali ya Bw. Ridhaa inapoteketezwa. Tukio hili ni mwongoni mwa matukio mengine mengi yanayoashiria ghasia katika utungo huu. Jambo hili limeshamiri katika riwaya ya Chozi la Heri kutoka mwanzo hadi mwisho. 4.7.1.6 Matumizi Mabaya ya Siasa Wahusika mbalimbali wa jinsia tofauti tofauti wamesawiriwa kama watu wanaoeneza siasa mbaya katika riwaya hii. Siasa ni sehemu muhimu ya maisha ya watu katika jamii. Kupitia kwa mchakato wa kisiasa ambapo jamii inaweza kujipatia uongozi ambao ni bora. Siasa mbaya husababisha kutovumiliana, ghasia na ukosefu wa utulivu na maendeleo katika jamii. Katika riwaya ya Chozi la Heri, masuala ya siasa mbaya yameendelezwa na wahusika mbalimbali baada ya uchaguzi wa kiongozi mkuu katika taifa la Uhafidhina. Baadhi ya viongozi na raia wa kiume wanaamini wana imani potovu kuwa uongozi ni kitu kilichoumbiwa wanaume na kwamba wanawake hawana wasaa na shughuli hii ya siasa. 41 Upotovu huu unaendelezwa na watu wenye taasubi ya kiume unaongozwa na mtetezi wao mkuu Mwanzi ambaye ni miongoni mwa watu wanaosababisha maafa katika taifa la Uhafidhina. Watu kama hawa hawathamini demokrasia kwani demokrasia huamini kuwa uongozi bora hutokana na kura za raia wala sio utajiri, ubabe, usugu, jinsia, kabila au dini. Katika riwaya hii, siasa mbaya inaenezwa na jinsia mbalimbali wanaoeneza ukabila na ubaguzi. Sababu yake ni kwamba Wahifidhina hawajatambua kuwa binadamu wote ni sawa na wanahitaji kuishi pamoja kwa amani bila mawazo ya ukoo na mbari ya kila mmoja. Wanasiasa wa jinsia mbalimbali wanang’ang’ania kura za raia na hawajali kuwaelimisha kuhusu mambo yanayoleta mshikamano wa kijamii. Isitoshe, wanasiasa hawa wanatumia ngazi ya ukabila kupanda mamlakani kwa kuwafanya watu wa jamii moja wachukie wale wa jamii zingine. Hii ndiyo sababu panapotokea mwanya katika uongozi wa taifa, watu wanapigana na kufukuzana kwa misingi ya kikabila. Suala hili linawafanya jinsia mbalimbali kukataa ndoa za kuvuka mpaka wa kikabila kama vile kisa cha Lucia bintiye Kangata ambapo kulitokea pingamizi asipate kuolewa na mtu wa jamii ya Waombwe ambao walichukuliwa kuwa maadui wa Anyamvua. Kwa mfano: Utamwozaje mwanetu kwa mtu wa ukoo ambao huvaa nguo ndani nje? Ukoo ambao unazaa majoka ya mdimu ambayo hata kiporo cha juzi hayawezi kukupa? Alisikika ami ya Lucia akilalamika. “Hao Waombwe msemao ndio waliomkuza Lucia wakati ambapo nyinyi nyote mliniita kidengereka. Bwana Kiriri aliyadhamini masomo ya mabinti zangu licha ya kujua kuwa sisi ni Nyamvua. Mlikuwa wapi wakati huo? Hizo tofauti zinakuja sasa hivi? Si nyinyi mliokuwa hata mkipinga elimu ya mabinti hawa? Hamkusema kwamba kuwapeleka shule ni kufisidi rasilimali? Leo sasa mnamwona mwanangu ametononoka si haba, na kuwa Mungu amemfungulia milango ya heri, ndio mnamthamini?” Kangata akaiambia jamaa yake (uk 66-67). Vilevile katika jamii ya Ndugu Kaizari, mkewe Subira aliye Mbamwezi hakupendwa na watu wa jamii alimoolewa, ikachangia kusambaratika kwa ndoa ya Ndugu Kaizari. 42 “Nasikia mama yangu ametoka kwenye jamii ya Bamwezi, baba mnajua jamii yake bila shaka. Daima mama alichukuliwa kama mgeni, si katika boma let tu, bali pia katika kijiji kizima. Haikuwa ibra kumsikia nyanya akimrejelea mama kama muki, yaani ‘Hiyo wa kuja’, na kusema kwamba msichana wa Bamwezi, hata akiwa na umri wa miaka tisini ni msichana wa Bamwezi tu. Haya yalilengwa kumkumbusha kwamba yeye hakuwa wetu. Uhasama ulizidi baada ya vurugu za miaka mitano iliyopita. Nyanya alimwona mama kuwa chanzo cha kuharibiwa kwa mali yetu, kwamba ndiye aliyewafanya majirani zetu kutuchomea boma ili watuondolee gugu ambalo liliutia najisi utambulisho wetu. Nilimtazama mama akidhoofika kiafya kwa majonzi ya kutengwa na wale aliowadhani ni aila yake. Sikujua kilichokuwa kinamdhili siku hizo, ila nilikisia kuwa mlikuwana mvutano kati yake, baba na nyanya” (uk 94-95). Familia ya kina Ridhaa ilipohamia Msitu wa Heri ni kama jamii za huko zilikuwa na wahka uliopelekea wao kuitwa Wafuata Mvua ambayo inasawiri ubaguzi wa kikabila. Ni siasa mbaya inayochangia mtibuko wa amani katika jamii zinazohamia Msitu wa Mto Mamba ambapo kunazuka mgawanyiko na uhasama wa kitabaka. Siasa mbaya inadhihirika katika kisa cha riwaya hii inahusiana na umilikaji wa ardhi. Aidha, wakaaji wa Mto Mamba hawajali uhifadhi wa mazingira ambayo ni hatari kwa ardhi. Misukosuko inapozuka, wanahamishiwa kwingine na serikali lakini watu wajanja serikalini wanaendelea kutumia hili eneo kisiri. Ni kama utawala unashtukia tu kuwa, kumbe mazingira ya eneo hili yalikuwa hatarini na hata hivyo hauchukui hatua madhubuti ya kurekebisha. 4.7.1.7 Kutowajibika Katika riwaya hii kuna baadhi ya wananchi wa Uhafidhina wanaosawiriwa kama watu wanaoshindwa kuwajibika mustakabali wa nchi yao na badala yake wanafuata kauli za kichochezi za wanasiasa kama Mwanzi ambaye anashikilia itikadi za kikale zisizo na mantiki katika dunia ya kisasa kama vile kuwa mtu wa kike hana wasaa na uongozi. Uchochezi wa wanasiasa kama hawa unatumbukiza taifa katika mitafaruku mibaya. Wafuasi wao hawataki kuwajibika bali wanawafuata kama vipofu na kulisukasuka taifa vibaya. 43 Baadhi ya wanawake waliosawiriwa kwa njia hasi katika riwaya hii ni pamoja na; Sauna, Naomi ambaye ni mkewe Lunga na mke wa Kiriri. Kwa mfano, kijakazi Sauna anawatorosha watoto Dick na Mwaliko. Aliyeajiriwa kuwatunza ndiye anayewapeleka utumwani. Huyu Sauna anashindwa kuwajibika katika jamii kwa kutumika kama nyenzo ya kuiletea jamii maafa ilhali kapewa kazi ya kuwatunza watoto. Naomi anasawiriwa kama mtu anayemtoroka mumewe Lunga pamoja na watoto kwa sababu zisizo na mantiki (uk 80-82). Hawa wahusika hawajibikii shughuli zao na wanaishia kuletea jamii majuto hata kupelekea watu wengine maafa. 4.7.1.8 Kutengwa kwa Watoto Katika riwaya ya Chozi la Heri watoto wanasawiriwa kama jinsia iliyotengwa na wenzao haswa kutokana na hali kuwa wamejifunza haya kutoka kwa wazazi wao. Ridhaa akiwa mdogo alitengwa na watoto wenzake katika mchezo wa kuvuta kwa madai kuwa alikuwa mfuata mvua, alikuwa mwizi na aliwashinda mtihani japo alikuwa mgeni. Msimulizi katika ukurasa wa 1 – 11 anasisitiza kuwa kwa ajili ya malezi mema Ridhaa hakuwajibu alishitakia hali yake kwa mamake. Mama akamhimiza kuishi na wenzake bila ubaguzi. Akamwelekeza Ridhaa kuwa elimu ilipaswa kuleta umoja miongoni mwa wanafunzi wala si chuki. Watoto hawa walisisitiziwa na mwalimu wao kuhusu umuhimu wa umoja na tangu hapo kutengwa kwa Ridhaa kukakoma, akapata ufanisi mkubwa katika elimu. 4.7.1.9 Watoto na Vijana Kuingizwa katika Ulanguzi wa Dawa za Kulevya Watoto na vijana mbalimbali katika riwaya hii wamesawiriwa kama watu ambao wanashirikishwa na hata kuuhusishwa katika biashara haramu ya kuuza na hata kutumia dawa za kulevya na matajiri. Vijana wa vyuo vikuu kwa kuwa na uhitaji waliangukia mtego wa kuuza dawa hizi na 44 pia kuzitumia (uk 142). Dick alihusishwa katika biashara hii akiwa na miaka kumi pekee. Akawa mraibu pia wa dawa hizi (uk 119 – 120). “Nasikia wanalewa kujipurukusha na hali duni ya maisha vyuoni. Wanasema kuwa gharama ya masomo imekuwa ghali, nayo halmashauri ya elimu inayotoa mikopo ya masomo haimudu kutosheleza mahitaji ya idadi kubwa ya wanafunzi wanaohitaji mikopo na ruzuku. Isitoshe, nasikia kwamba wanaoishia kupewa mikopo au ruzuku hizi ni watoto kutoka familia zinazojiweza kiuchumi huku wana wa maskini wakilazimika kufanya vibarua wakati wa likizo kujilipia karo na kugharamia mahitaji mengine. Wengine huwa mawindo rahisi ya matajiri wanaotafuta roho za kulangulia na kusafirishia dawa za kulevya ughaibuni,” Meko akachangia (uk 142). Miaka kumi ya adha na mashaka imepita. Sasa Dick emekomaa. Ilibidi akomae kwani ulimwengu haukuhitaji ‘mtoto wa mama’, kama alivyozoea kumwambia kijakazi Sauna ambaye alimtosa katika kinamasi hiki cha kulangua dawa za kulevya. Dick amesafirisha maelufu kwa maelufu ya vifurushi vya dawa hizi. Mwanzoni hakuwa mraibu wa dawa hizi lakini ilibidi ajizoeshe, kwa usalama wake mwenyewe, kwani mara nyingi ilibidi kuzimeza dawa zenyewe ili kwenda kuzitapika kwenye masoko ughaibuni. Hili lilitokea wakati mashine za forodhani zilipopata makali zaidi siku nyingine na kung’amua shehena ambazo zilikuwa zimeshonewa vibindoni! (uk 119 – 120). 4.7.2 Ukandamizaji wa Kijinsia katika Maisha Kitendawili Suala la ukandamizaji wa jinsia mbalimbali linatokea katika riwaya ya Maisha Kitendawili. Jambo hili linatokea kwa njia mbalimbali katika riwaya hii. Mifano ni kama ifuatayo: 4.7.2.1 Kutelekezwa kwa Mwanamke katika Ndoa Katika riwaya ya Maisha Kitendawili, jinsia ya kike amesawiriwa kama mtu aliyetelekezwa katika ndoa. Sababu yake ni kwamba majukumu yote yanayostahili kutekelezwa na jinsia ya kiume yametwikwa ama ni majukumu yaliyowachiwa jinsia ya kike. Suala hili ni kisababishi cha changamoto mbalimbali zinazowakumba wanawake katika ndoa katika jamii. Kwa mujibu wa Ayis (1979:9) jinsia ya kiume inatambulishwa na utamaduni katika ndoa kama jinsia inayostahili kulisha familia yake na kuwa kuna usalama wa watoto pamoja na mama yao. Hivyo basi, jinsia ya 45 kike hatarajiwi kuwachiwa majukumu yote ya kinyumbani kama vile kulisha familia yake kama anavyofanya jinsia ya kiume katika riwaya hii. Jinsia ya kiume kama vile Mzee Omar katika riwaya ya Maisha Kitendawili anatambulishwa kama jinsia isiyotekeleza wajibu wake wa kifamilia katika ndoa. Kwa kuwa mzee huyu alikuwa anaugua maradhi ya puma tangu utotoni, mkewe ndiye anayechukua wajibu ama majukumu yote ya kinyumbani. Vilevile mkewe Mzee Omari anajengwa kama jinsia inayotafuta hata hela za kumpeleka mumewe kwa Mganga Kalulu wakati anapozidiwa na maradhi. Mfano katika riwaya: Japo hakuwa na kazi na aliendeshwa na mkewe alikuwa mkulima madhubuti (uk. 32). Mwanamke mwingine anayetambulishwa kama jinsia iliyotelekezwa katika ndoa ni Rose. Mwanamke huyu anasawiriwa kama mchuma riziki katika familia yake kwa sababu mumewe hana uwezo wa kufanya hivyo. Rose anamsimulia Farida yafuatayo katika riwaya hii: “wajua nilikuwa katika umaskini wa kutosha. Baba yangu ana mkono mmoja na mama hana kazi. Mama ndiye anayejaribu kutulea. Kila siku tulikula mboga za majani mpaka jirani zetu wakatubandikia majina” (uk. 105). Isitoshe, Mama Josii ambaye ni muhsika katika riwaya hii pia anasawiriwa kama jinsia iliyowachiwa majukumu yo