Thesis: Nafasi ya fasihi katika kuwasilisha masuala ya mazingira kupitia riwaya teule tikitimaji (2013) na msimu wa vipepeo (2006) za K.W Wamitila
Authors
Wesonga, Lucy EstherAbstract
Suala la mabadiliko ya hali ya anga ni janga linaloendelea kukumba ulimwengu kwa jumla. Kutokuwepo kwa usawazishaji wa ikolojia ni jambo ambalo linawatia shaka adinasi wengi. Fasihi ni kioo cha jamii na inapaswa kuwasilisha hali halisi ya maisha ya binadamu. Utafiti huu ulichambua nafasi ya fasihi katika kuwasilisha masuala ya mazingira kupitia riwaya mbili teule za wamitila, Tikitimaji (2013) na Msimu Wa Vipepeo (2006). Niliteua riwaya za Wamitila kwa sababu mwandishi huyu ameonyesha ari katika uwanja wa fasihi mazingira, kwenye makala yake ya “place and placelessness in Kiswahili literature: The role of setting in Kiswahili creative writing” (1999), anasema kuwa mandhari huchukua nafasi katika kuwasilisha masuala ya mazingira. Hivyo utafiti ulichunguza namna alivyotumia fasihi kuwasilisha masuala ya mazingira katika riwaya zake. Ingawa kwa miaka mingi, masuala ya mazingira yamehusishwa na sayansi haswa katika kutoa takwimu kamilifu kuhusiana na masuala ya mazingira, fasihi inaendelea kuchukua dhima mpya katika jamii inayozidi kukua kiteknolojia. Utafiti huu uliongozwa na madhumuni yafuatayo: kubainisha jinsi mwandishi wa riwaya ya Tikitimaji alivyotumia wahusika ili kuwasilisha maudhui ya mazingira; pili, kueleza mitindo ya lugha iliyotumiwa kuwasilisha masuala ya mazingira na tatu, kutathimini iwapo mwandishi amefaulu kuwasilisha maudhui ya mazingira riwayani. Utafiti huu ulitumia kiunzi cha nadharia kutoka kwa nadharia ya fasihi mazingira na nadharia ya uhalisia. Mihimili zilizotumiwa kutoka kwa nadharia ya uhalisia ni: kazi ya fasihi imejitosheleza, kazi ya msanii inapaswa kuwasilisha ukweli, mtunzi anaangalia matatizo na kuchunguza chanzo chake na mwisho wahusika ni vielelezo yakini vya binadamu wa kawaida kwa vile wao hutumia lugha ya kawaida wanayoitumia humwezesha mwanadamu kujifafanulia uwezo wake wa kutenda mambo. Kutoka kwa nadharia ya fasihi mazingira, mihimili ifuatayo ilitumika: fasihi inapaswa kuwasilisha mielekeo ya binadamu kuhusu mazingira, kuangalia matumizi ya dhana za ekolojia katika kazi za kifasihi, nguvu za kibinadamu na lugha ya binadamu kuhusiana na mazingira, huangalia mitindo ya lugha na jinsi mitindo hiyo huathiri namna binadamu anavyotagusana na mazingira na mwisho huchukulia kuwa mazingira na utamaduni hushirikiana katika ujenzi wa lugha na fasihi, binadamu hawezi kuishi bila ekolojia lakini ekolojia huweza kuishi bila binadamu pia huangalia jinsi waandishi huwakilisha masuala ya mazingira na jinsi kazi hiyo huathiri mielekeo ya ulimwengu katika hali halisi. Muundo wa utafiti ulikuwa ni wa kiuchanganuzi. Utafiti ulifanywa maktabani. Riwaya za Wamitila, Tikitimaji (2013) na Msimu Wavipepeo (2006) ndizo zilizoteuliwa kimakusudi kama sampuli ya utafiti huu. Data ilipangwa kwenye makundi na kuchanganuliwa kwa kuzingatia madhumuni ya utafiti na mihimili ya kiunzi cha nadharia. Data iliwasilishwa kwa njia ya maelezo. Utafiti huu ulilenga kuhamasisha wasomi na waandishi wa fasihi wajikite zaidi kulenga masuala ya mazingira ambayo ndicho kitovu cha maisha ya binadamu. Utafiti ulibaini kuwa fasihi ni nyenzo mwafaka ya kuwasilisha masuala ya mazingira kupitia vipengele vyake. Hii ni kwa sababu fasihi huingiliana sana na utamaduni wa jamii.
Cite this Publication
Usage Statistics
Files
- Total Views 56
- Total Downloads 38