Thesis: Kuchanganua makosa ya kimofofonolojia katika kazi andishi za kiswahili miongoni mwa wanafunzi wenye asili ya lugha ya kikuyu katika shule za upili: Kahuro, Murang’a
Authors
Juliet Aswani MukhwanaAbstract
Lugha yoyote ya kwanza kwa kawaida huwa na athari wakati wa harakati za kufahamiana na lugha nyingine. Hiki ndicho chanzo cha ukosaji wa Kiisimu kati ya wanagenzi wanaojifunza lugha ya pili. Hivyo, wanagenzi wengi wa lugha ya Kiswahili hawajaachwa nyuma. Wengi wao wameathirika si haba.Wao hujikuta kwenye makosa yaya haya kwa kuhamisha ruwaza ya Kiisimu ya lugha wanayoimiliki hadi kwa lugha ya pili ambayo ni Kiswahili. Mada ya uchunguzi huu ni uchanganuzi wa makosa yanayohusiana na mofofonolojia kwenye kazi andishi za Kiswahili miongoni mwa wanagenzi wenye asili ya lugha ya Kikuyu katika shule za sekondari: Kahuro, jimbo la Murang’a. Malengo mahususi ni kubainisha ukosaji wa kifonolojia kwenye kazi andishi za Kiswahili miongoni mwa wanagenzi hawa katika jitihada zao za kujifunza lugha ya Kiswahili, kutambua ukosaji wa kimofolojia kwenye kazi andishi za Kiswahili ambao unafanywa na wanagenzi hawa katika ujifunzaji wao wa lugha ya Kiswahili, kubaini asili ya ukosaji wa umofofonolojia katika kazi andishi za Kiswahili katika juhudi za ujifunzaji wa lugha ya Kiswahili na kutathmini namna ya kurekebisha ukosaji wa kimofofonolojia kwenye kazi andishi za lugha ya Kiswahili kati ya wanagenzi hawa. Ili kufikia malengo haya, mtafiti alijikita kwenye wanagenzi wa shule za sekondari za kutwa katika jimbo dogo la Kahuro lililo katika jimbo la Murang’a. Pia, mtafiti alifanya utafiti maktabani kuchunguza hali ya makosa kwenye lugha tofauti tofauti na pia vyanzo vya makosa na jinsi ya kurekebisha makosa hayo katika lugha. Data ambayo ilikusanywa kwenye uchunguzi huu ni ya aina ya kithamano ambapo makosa ya kifonolojia na kimofolojia katika insha yalibainishwa na kuchanganuliwa kwa kutumia maelezo kulingana na vigezo vya Nadharia ya Uchanganuzi Makosa iliyoanzishwa na mtaalamu Corder katika mwaka wa 1960. Uchunguzi huu ni wa aina ya kimaelezo na ulitekelezwa nyanjani na pia katika maktaba. Sampuli ya uchunguzi huu ilichaguliwa kwa kutumia njia za kimakusudi. Sababu ya kutumia mbinu hii ni kuwa ililenga shule za upili za kutwa katika jimbo dogo la Kahuro, kaunti ya Murang’a ili kupata data kuhusu ukosaji wa kimofofonolojia unaofanywa na wanagenzi wa shule za sekondari katika kazi andishi za Kiswahili. Baada ya data kukusanywa ilichanganuliwa kwa kutumia mbinu ya kimaelezo kwa mujibu wa mihimili ya Nadharia ya Uchanganuzi Makosa na pia madhumuni ya utafiti huu kama yalivyotajwa hapo juu. Kwenye sura ya kwanza, tumeangazia usuli wa mada, suala la uchunguzi, madhumuni ya utafiti, maswali ya uchunguzi, sababu za kuchagua mada, umuhimu wa uchunguzi pamoja na kufafanua istilahi muhimu. Katika sura ya pili tumeangazia mwauo wa maandishi na misingi ya nadharia ambayo iliongoza utatifi. Katika sura ya tatu, mbinu za uchunguzi, mahali pa uchunguzi, uteuzi wa sampuli, vifaa vya utafiti, kukusanya data, kuchanganua data na maadili ya utafiti yameshughulikiwa. Sura ya nne nayo imeshughulikia maelezo ya kimsingi kuhusu fonolojia, mofolojia mofofonolojia, mifanyiko ya kimofofonolojia, sauti za Kiswahili na Kikuyu, uwasilishaji na uchanganuzi wa data iliyokusanywa ilhali ile ya mwisho inahusu muhtasari, matokeo na pia mapendekezo ya utafiti huu.
Cite this Publication
Keywords
Usage Statistics
Files
- Total Views 0
- Total Downloads 13