Thesis: Mtindo wa nyimbo za injili za christopher nyangwara mosioma (embarambamba) mwaka 2021- 2023
Authors
Kiunga Jonah KesiAbstract
Nyimbo ni moja wapo wa tanzu za Fasihi zinazopatikana miongoni mwa wanajamii. Kuna mifano mingi ya aina ya nyimbo za dini zinazotumika katika shughuli mbalimbali za kuabudu na kumtukuza Mungu. Nyimbo hizi zina majukumu muhimu yanayoendana na mambo ya dini, haswa za shughuli za ibada. Katika hali ya kawaida, nyimbo hutungwa kwa ustadi wa kiwango cha juu cha lugha. Tasnifu hii imejadili mtindo katika kuwasilisha ujumbe kwenye nyimbo za Christopher Nyangwara Mosioma msanii wa nyimbo za injili nchini Kenya almaarufu Embarambamba. Utafiti huu umeainisha, kutambulisha na kufafanua vipera vya kimtindo vinavyotumiwa na mwanamuziki Christopher Nyangwara Mosioma anapotunga nyimbo zake na pia kuangazia maudhui ambayao huambatana moja kwa moja na mtindo anaoutumia msanii kwenye kuumba kazi yake. Utafiti huu umejikita katika vipengele vinne; mtindo, msuko, maudhui na matumizi ya lugha. Utafiti huu ulilenga kufanikisha lengo moja kuu na malengo matatu maalumu ambayo ni; Kuainisha msuko wa maudhui, Kuchanganua matumizi ya lugha na la mwisho ni kutathmini athari za mtindo wa msuko wa maudhui na matumizi ya lugha katika nyimbo za injili za Christopher Nyagwara Mosioma (Embara mbamba) mwaka 2021- 2023. Maswali ya utafiti yalikuwa; Je, ni maudhui yapi yanayopatikana katika nyimbo za Christoppher Nyangwara Mosioma? Ni mtindo upi wa matumizi ya lugha unaojitokeza katika nyimbo za injili za Christopher Nyangwara Mosioma? Na je, mtindo wa msuko wa maudhui na matumizi ya lugha katika nyimbo za Christopher Nyangwara Mosioma una athari gani katika jamii? Nadharia iliyotumika ni Nadharia ya Simiotiki inayojishughulisha na ishara pamoja na hali ya kuashiria kwenye utunzi wa Fasihi. Uteuzi wa sampuli kimaksudi ulitumika katika ukusanyaji wa data. Data yenyewe ilinakiliwa kwa kurejelea malengo ya utafiti na msingi wa nadharia husika. Utafiti wa maktabani ulitumika kwa ukusanyaji wa data kwa kusoma tasnifu za awali, vitabu na matini za mtandaoni ambazo zilisaidia kuafikiwa kwa malengo ya kazi hii. Matokeo ya utafiti huu yameandikwa kwa kufuata muundo wa wa kimaelezo. Data yenyewe ilikusanywa kwa njia moja kuu ya usikilizaji makini wa nyimbo husika za msanii teule na kudondolewa kwa vipengele vinavyohitajika na kuandikwa. Umuhimu wa utafiti huu ni kuwa, wasanii watanufaika pakubwa katika kuzijenga kazi zao za kisanii kwa weledi na ufundi mkubwa na hata matokeo ya kazi hii pia, yatatumika kama moja wapo ya vipengele yva kubainisha pengo la maarifa litakalojazwa na utafiti huu. Matokeo ya utafiti huu pia yatawafaa pakubwa watafiti na wasomi kwa kupata marejeleo katika uwanja huu wa utafiti huu uliofanywa.
Cite this Publication
Keywords
Usage Statistics
Files
- Total Views 0
- Total Downloads 1