Thesis:
Shujaa pwaya katika riwaya ya kidhanaishi: mfano wa riwaya teule za euphrase kezilahabi

Abstract

Kuwepo wa shujaa pwaya katika fasihi si jambo lililozuka hivi karibuni. Ushahidi wa kihistoria unabainisha kuwepo kwa shujaa pwaya katika tamthilia ya urasimi mkongwe wa Kiyunani. Utafiti huu ulichunguza usawiri wa shujaa pwaya katika riwaya teule za kidhanaishi za Kiswahili zilizotungwa na Euphrase Kezilahabi ambazo ni: Kichwamaji (1974), Dunia Uwanja Wa Fujo (1975) na Rosa Mistika (1971). Mtafiti alilenga kutathmini usawiri wa shujaa pwaya katika riwaya teule zilizochunguzwa. Aidha, utafiti uliazimia kuchunguza ujumbe muhimu unaowasilishwa kupitia kwa shujaa pwaya katika riwaya teule zilizochanganuliwa. Istitoshe, utafiti ulikusudia kutathmini dhima ya shujaa pwaya katika riwaya teule zilizochambuliwa. Utafiti huu ulikuwa wa maktabani. Riwaya tatu zilizoshirikishwa katika utafiti huu ziliteuliwa kwa kuzingatia usampulishaji wa kimaksudi. Mtafiti alisoma kwa kina riwaya sita za Kezilahabi na kutumia kigezo cha kuwepo kwa shujaa pwaya kuchagua riwaya tatu zilizochanganuliwa katika utafiti huu. Mtafiti alichanganua riwaya teule zilizoshirikishwa katika utafiti huu akiongozwa na mihimili ya Nadharia ya Udhanaishi iliyoasisiwa na Soren Kiekergaard. Nadharia ya Udhanaishi hujishughulisha na hali ya maisha ya binadamu kwa mtazamo wa falsafa ya kidhanaishi. Swali muhimu katika nadharia hii huwa ‘maisha nini?’ Wadhanaishi hutafiti na kusaili kwa kina uwepo na hatima ya binadamu duniani. Mbinu ya utafiti iliyotumika katika utafiti huu ni ile ya utafiti wa maktabani. Data iliyokusanywa ni ya kithamano. Data ya kithamano ilichanganuliwa na kufasiriwa kwa kutoa maelezo kwa mujibu wa mihimili ya Nadharia ya Udhanaishi. Maelezo ya kiufafanuzi yalitolewa kuhusu mbinu zilizotumika kusawiri shujaa pwaya pamoja na dhima yake katika kuwasilisha ujumbe muhimu karika riwaya teule. Matokeo ya utafiti yanabainisha kuwa shujaa pwaya amesawiriwa kama aliye na fikra za kimapinduzi, mwasi wa nguzo za kimaadili katika jamii yake na aliyegubikwa na unyume. Baadhi ya ujumbe muhimu unaowasilishwa kupitia kwa shujaa pwaya unahusu malezi, uozo wa maadili, utamaushi, uhuru wa mtu binafsi na nafasi ya mwanamke katika jamii. Dhima kuu ya shujaa pwaya ni kutekeleza majukumu ya kimsingi yanayokuza vipengele vya fani na maudhui katika riwaya husika. Utafiti huu utakuwa na mchango hasa kwa upande wa kuendeleza mbinu za mtindo kwa waandishi chipukizi wanaokusudia kutunga fasihi ya kidhanaishi. Aidha, matokeo ya utafiti yanatoa mwanga kuhusu usawiri wa shujaa pwaya katika riwaya ya kidhanaishi.

Cite this Publication
Abaya, W. O. (2025). Shujaa pwaya katika riwaya ya kidhanaishi: mfano wa riwaya teule za euphrase kezilahabi. Mount Kenya University. https://erepository.mku.ac.ke/handle/123456789/7272

Keywords

Usage Statistics

Share this Publication

  • Total Views 0
  • Total Downloads 2

Journal Title

Journal ISSN

Volume Title

Publisher

Mount Kenya University