Thesis: Usawiri wa ugonjwa, uuguzi na tiba katika methali za kiswahili
Authors
Joseph Gikonyo MwangiAbstract
Tangu jadi, binadamu amekumbwa na magonjwa hatari yaliyokuwa changamoto katika maisha yake. Kwa hivyo, wanajamii wamekuwa wakitafuta njia za kuuguza na kutibu magonjwa ya kila aina. Utafiti huu unahusu nafasi ya methali za Kiswahili katika kusawiri ugonjwa, uuguzi na tiba yake. Methali ni kipera muhimu cha utanzu wa semi katika fasihi simulizi. Methali ni hazina kubwa katika maisha ya wanajamii kwani zinasheheni dhima mbalimbali katika jamii inayohusika. Mojawapo ya dhima hizo ni kusawiri hali mbalimbali zinazowazunguka wanajamii, yakiwemo magonjwa yanayowakumba, uuguzi na jitihada za kutafuta tiba mujarabu ya magonjwa haya. Utafiti huu umechochewa na uhalisi kwamba, ingawa methali za Kiswahili zimechunguzwa, kuorodheshwa na kuainishwa kwa kategoria mbalimbali kwa mujibu wa miktadha na dhima zake, bado kuna pengo la maarifa katika uchunguzi wa usawiri wa magonjwa, uuguzi na tiba katika kuwasilisha ujumbe wa methali hizi. Utafiti huu unajikita katika malengo matatu mahususi: kwanza, kufafanua matumizi ya vipengele vya fani kubainisha ugonjwa, uuguzi na tiba katika methali za Kiswahili. Pili, kudadavua matumizi ya ugonjwa, uuguzi na tiba kuwasilishia ujumbe katika methali za Kiswahili na tatu kutathmini athari ya usawiri wa ugonjwa, uuguzi na tiba kwa ufasiri wa ujumbe wa methali za Kiswahili. Uchunguzi huu uliokitwa katika muundo wa kimaelezo unaongozwa na nadharia ya Semiotiki iliyoasisiwa na Ferdnand De Saussure na Charles Pierce. Vyanzo vya methali zinazochambuliwa ni kamusi 3 za methali - Maelezo ya Methali za Kiswahili, Kamusi ya Methali na Kamusi ya Methali: Maana na Matumizi. Sababu ya kuteuliwa kwa kamusi hizi ni kuwa zinaafikiana na azma kuu, malengo na nadharia ya utafiti. Usampulishaji lengwa ndio uliotumiwa kuteua kamusi pamoja na methali zinazohusu ugonjwa, uuguzi na tiba katika kamusi teule. Idadi lengwa ni methali 5,856 kwenye kamusi teule. Kati ya methali hizi, 90 ndizo zilizoteuliwa kwa sababu zinaakisi malengo ya utafiti. Njia za ukusanyaji wa data maktabani ambazo ni kusoma tasnifu mbalimbali, vitabu na makala mbalimbali yanayohusiana na mada ya utafiti huu, ndizo zinazotumiwa kuufanikisha utafiti huu. Matokeo ya utafiti huu yanadhihirisha kwamba, methali za Kiswhili zinazosawiri ugonjwa, uuguzi na tiba zinatumia vipengele vya fani kama vile takriri, kinaya, taswira, kejeli, tashihisi na sitiari kuwasilishia ujumbe wake. Vipengele hivi vya fani ndivyo vitumikavyo kuufumba na kuukoleza ujumbe wake. Pia imethibitika kwamba methali za Kiswahili zinazosawiri ugonjwa, uuguzi na tiba zinatumika kuwasilisha ujumbe maalum kama vile jumbe zilizoza matumaini, utamaushi, tahadhari, subira pamoja na kuhamasisha upendo, umoja na ushikamano katika jamii. Hatimaye, athari chanya na hasi zinazotokana na ufasiri wa ujumbe katika methali hizi zinajitokeza vyema kama vile: umuhimu wa kufanya mambo kwa utaratibu, uhusiano wa karibu uletwao na ugonjwa, ukataji shauri, usiri mtu anapougua, ustahamilivu, ubaguzi na unyanyapaa, makovu ya ugonjwa maishani, msaada, matumaini pamoja na uchungu uletwao na baaadhi ya magonjwa unadhihirishwa. Kutokana na dhima yake kuadilisha vijana na jamii nzima, inapendekezwa methali zihifadhiwe ili kudumisha ujumbe ulio kwenye methali hizi. Ili kuelewa ujumbe wake, muundo wa tungo na maneno ya methali uzingatiwe kwa kina. Utafiti huu una tija kwa wasomi wa fasihi, hususan wenye raghba ya methali kwa sababu umefafanua jinsi ugonjwa, uuguzi na tiba unafanikisha na/kuathiri ufasiri na welewa wa methali za Kiswahili. Matokeo ya utafiti huu yatawawezesha watunzi wa kazi za fasihi kuelewa jinsi ya kuutambua ujumbe wa ndani uliofumbatwa kwenye methali hizi ili kuzitumia ifaavyo. Kwa watafiti, matokeo ya utafiti huu ni msingi na chachu ya uchunguzi wa baadaye.
Cite this Publication
Usage Statistics
Files
- Total Views 1
- Total Downloads 1